Syria: Marekani iko safu moja na magaidi kupambana na serikali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27416-syria_marekani_iko_safu_moja_na_magaidi_kupambana_na_serikali
Ikulu ya Rais Bashar al-Assad wa Syria imesema kuwa, mashambulizi ya Marekani dhidi ya kambi ya kikosi cha anga cha nchi hiyo katika eneo la Shayrat, mashariki mwa Syria ni hatua ya kijinga na inayotokana na mtazamo finyu wa kisiasa na kijeshi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 07, 2017 08:39 UTC
  • Syria: Marekani iko safu moja na magaidi kupambana na serikali

Ikulu ya Rais Bashar al-Assad wa Syria imesema kuwa, mashambulizi ya Marekani dhidi ya kambi ya kikosi cha anga cha nchi hiyo katika eneo la Shayrat, mashariki mwa Syria ni hatua ya kijinga na inayotokana na mtazamo finyu wa kisiasa na kijeshi.

Taarifa iliyotolewa leo na ikulu ya rais wa Syria imesema kuwa, hujuma hiyo ya Marekani ni uvamizi wa kidhalimu ulio wazi na kwamba, mienendo ya kindumiakuwili ya Washington ndiyo imeifanya nchi hiyo kufanya kitendo hicho cha kijinga nchini Syria. Wakati huo huo Bouthaina Shaaban, Mshauri wa Rais wa Syria katika masuala ya Habari na Siasa amesema kuwa, shambulizi la Marekani nchini humo limemuondolea shaka kila mtu kwamba Washington iko safu moja na magaidi katika kupambana na serikali ya Syria.

Manuwari ya Marekani ikifyatua makombora kushambulia Syria

Shaaban ameyasema hayo leo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Mayaadin na kuongeza kuwa, mashambulizi hayo ya Marekani yametelekelezwa baada ya jeshi la Syria kupata ushindi mkubwa mkoani Hama ulioenda sambamba na kufurushwa magaidi ambao walikuwa wanakusudia kushambulia mji mkuu wa nchi hiyo Damascus. Mshauri wa Rais Bashar al-Assad katika masuala ya Habari na Siasa amefafanua kuwa, Msyria yeyote anayeunga mkono hujuma hizo za Marekani dhidi ya taifa hilo la Kiarabu, ni haini kama ambavyo pia nchi za Kiarabu zinazoyadhaminia fedha makundi ya kigaidi yanayofanya jinai nchini Syria, Yemen Iraq na Libya, hazina utambulisho wa Kiarabu.

Bouthaina Shaaban, Mshauri wa Rais wa Syria katika masuala ya Habari na Siasa

Wakati huo huo, Mohammad Ramez Tourjman, Waziri wa Habari wa Syria amesema kuwa, mashambulizi ya Marekani nchini humo ni matumizi mabaya ya madaraka ya kisiasa. Amesema kuwa, huko nyuma utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulishambulia mara kadhaa maeneo ya jeshi la Syria na hii leo pia Marekani imetekeleza hujuma hizo kwa lengo la kukamilisha lile ambapo Israel ilishindwa kulikamilisha.

Sehemu nyingine ya hujuma za kijuba za Marekani katika kuwasaidia magaidi

Amefafanua kuwa, hivi sasa Syria inakabiliwa na mashambulizi ya kila upande yakiwemo ya kisiasa, kijeshi, kiuchumi kutoka zaidi ya nusu ya nchi zote za ulimwengu. Jumla ya Wasyria 10 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa leo alfajiri, katika mashambulizi ya Marekani yaliyolenga kambi ya kikosi cha anga cha jeshi la Syria ya Shayrat, mashariki mwa mkoa wa Homs.