Marekani yaua zaidi ya raia 200 nchini Syria
Ndege za kivita za Marekani zimeua raia wasiopungua 204 tangu mwezi Machi hadi hivi sasa katika mashambulizi ya anga yanayofanywa na nchi hiyo huko Raqqah, kaskazini mwa Syria.
Mtandao wa habari wa al 'Ahd wa Lebanon umelinukuu kundi linalodai ni la haki za binadamu lililo karibu na magaidi wa Syria likitangaza jana kwamba, watoto 32 na wanawake 34 wameuawa kati ya raia 204 waliouliwa kwenye mashambulizi ya anga ya Marekani katika mji wa Raqqah na viunga vyake.
Takwimu zinaonesha kuwa wahanga wakubwa wa mashambulizi ya Marekani inayodai kupambana na magaidi wa Daesh nchini Syria, ni raia wa kawaida.
Mgogoro wa Syria ulianzishwa mwaka 2011 baada ya magaidi kutoka kila kona ya dunia kumiminwa nchini Syria kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Kiarabu na kwa kutumia nguvu za Marekani na nchi jirani kama Uturuki.
Uvamizi huo umesababisha hasara kubwa za roho na mali nchini Syria na kila leo uadui dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu ambayo ni mpinzani mkubwa wa Israel, unafanyika kwa sura tofauti.