May 29, 2017 07:11 UTC
  • Ghasia mpya Bahrain, Sheikh Qassim hajulikani aliko

Askari wa utawala wa kiimla wa Bahrain wameendelea kuwashambulia wananchi wanaoandamana kumuunga mkono mwanazuoni wa Kiisalmu Sheikh Isa Qassim ambaye sasa ametoweka na hajulikani aliko.

Taarifa zinasema wanajeshi waliwashambulia wananchi waliokuwa wakiandamana kwa amani katika Kisiwa cha Sitra huku wakitoa nara dhidi ya utawala wa ukoo wa Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa Jumapili usiku. Aidha maandamano yamefanyika katika  mji wa Bilad Al Qadeem na vijiji vya Shahrkan, Samaheej, Bani Jamra, Musalla, Karranah, Karzakan, Karbabad, Daih na Sanabis.

Waandamanaji waliulaani vikali utawala wa Aal Khalifa kwa jinai zake katika kijiji cha Diraz kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ambapo waandamanaji kadhaa waliuawa shahidi wakati jeshi lilipovamia nyumba ya mwanazuoni mtajika wa Kiislamu Sheikh Isa Qassim. Mashahdi hao walizikwa Ijumaa pasina familia zao kutoa idhini katika kitendo kilichotajwa kuwa ni jinai.

Mei 23, askari wa Bahrain wakisaidiwa na wanajeshi wa Saudia na Imarati walivamia kijiji cha Diraz ambacho kimekuwa chini ya mzingiro kwa mwaka mmoja sasa na kuhujumu nyumba ya Sheikh Qassim, kiongozi wa kiroho wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao ndio wengi nchini Bahrain.

Waandamanaji Bahrain wakiwa wamevaa sanda wakiandamana dhidi ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa

Waandamanaji watano waliuawa shahidi katika hujuma hiyo. Maandamano hayo yalianza Mei 21 wakati mahakama ya kimaonyesho Bahrain ilipotoa hukumu ya kumfunga Sheikh Qassim mwaka mmoja gerezani na kumuamuru alipe faini ya  $265,266. Mwaka jana Sheikh Qassim alipokonywa uraia wake kutokana na harakati zake za kupinga utawala wa kiimla nchini humo.

Wakati huo huo hivi sasa hatima ya Sheikh Qasim haijulikani huku kukiwa na ripoti kuwa utawala wa kifalme unalenga kumtuma uhamishoni ima nchini Uturuki au Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya Waziri Mkuu wa Iraq Haider al Abadi kukataa ombi la kubaidishwa mwanazuoni huyo nchini humo.

Tokea tarehe 14 Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati ya mwamko wa Kiislamu dhidi ya ukandamizaji na mbinyo wa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi. Utawala huo ukiwa na lengo la kuzima sauti na cheche za moto wa malalamiko hayo umewatia mbaroni wanaharakati wa kisiasa, vijana na raia wengine wa nchi hiyo na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela.

 

Tags