Kuakisiwa kimataifa mafanikio ya jeshi la Syria dhidi ya magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31100-kuakisiwa_kimataifa_mafanikio_ya_jeshi_la_syria_dhidi_ya_magaidi
Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, kundi la kigaidi la Daesh limo katika hali ya kurejea nyuma kufuatia mashinikizo ya jeshi la Syria.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jun 29, 2017 02:51 UTC
  • Kuakisiwa kimataifa mafanikio ya jeshi la Syria dhidi ya magaidi

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, kundi la kigaidi la Daesh limo katika hali ya kurejea nyuma kufuatia mashinikizo ya jeshi la Syria.

Staffan de Mistura amesema kuhusiana na kuanzishwa maeneo ya kupunguza vita na mapigano nchini Syria kwamba, kuna jitihada zinazofanyika katika uwanja huo. De Mistura ameongeza kuwa, mkutano ujao wa Astana mji mkuu wa Kazakhstan utaendeleza ajenda ya kuanzisha maeneo ya kupunguza vita nchini Syria. Inaelezwa kuwa, kutokana na magaidi nchini Syria kushindwa kufikia malengo yao na kupokonywa fursa ya kuendeleza jinai zao, umepatikana uwanja na mazingira ya kutekelezwa mpango wa kuanzisha maeneo ya kupunguza vita na mapigano katika nchi hiyo.

Hadi sasa kumefanyika duru nne za mazungumzo ya amani ya Syria katika kiwango cha juu katika mji wa Astana kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa serikali ya Damascus na makundi ya wabeba silaha. Aidha moja ya natija za mazungumzo hayo ni kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita huku nchi za Iran, Russia na Uturuki zikiwa ziko mstari wa mbele kudhamini amani katika nchi hiyo ya Kiarabu. Moja ya matunda makuu ya mazunguzmo ya Astana ni kutiwa saini hati ya kuanzisha maeneo ya kupunguza vita na mapigano nchini Syria.

Staffan de Mistura, Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria

Duru zote hizo za mazungumzo zimefanyika kwa ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikishirikiana na Russia na Uturuki, lengo hasa likiwa ni kurejesha amani na uthabiti nchini Syria.

Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo kuhusiana na Syria yaliyokuwa yakifuatiliwa na Magharibi yakiwemo ya Geneva, hadi sasa hayajawa na natija yoyote ile kutokana na kufuatiliwa malengo machafu ya kuwaunga mkono magaidi wa Syria.

Mgogoro wa Syria uliibuka mwaka 2011 baada ya magaidi wanaoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wake ikiwemo Uturuki kuanzisha mashambulio kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais Bashar al-Assad. Hata hivyo kusimama kidete jeshi na wananchi wa Syria mbele ya njama dhidi ya taifa hilo kivitendo kumekwamisha njama za maadui hao na kuvuruga mahesabu yao yote.

Jambo hilo kivitendo limewafanya walimwengu washuhudie vipigo na kushindwa mtawalia magaidia huko Syria na hatimaye kulazimika kurejea nyuma na kukimbia kutoka katika nchi hiyo.

Jeshi la Syria

Wakati Syria ilipokuwa ikikabiliwa na wimbi kubwa la njama yakiwemo mashambulio makubwa ya magaidi wanaoungwa mkono na Magharibi, ilikuwa ikionekana kuwa, ni jambo lililo mbali kwa Syria kuweza kuvuka kipindi hicho kigumu na hatari.

Hasa kwa kutilia maanani kwamba, duru za Magharibi zilikuwa zikiendesha propaganda kubwa na kuwaonyesha walimwengu kwamba, utawala wa Rais Assad umefikia ukingoni. Lililo wazi ni kwamba, madola ya Magharibi yalipuuza na kutozingatiwa katika mahesabu yao azma na irada ya jeshi na wananchi wa Syria katika kupambana na njama dhidi ya taifa lao.

Ala kulli haal, mafanikio ya jeshi la Syria na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo yamefungua ukurasa mpya katika historia ya muqawama na mapambano ya nchi hiyo ya Kiarabu tukio ambalo limeakisiwa pakubwa kimataifa.

Rais Bashar al-Assad wa Syria

Hapana shaka kuwa, kushindwa magaidi nchini Syria na Iraq ni utangulizi wa ushindi zaidi wa jamii ya kimataifa mbele ya ugaidi na nukta ya msingi hapa ni kudhihirika mchango na nafasi ya mapambano ya wananchi na nguzo za ulinzi wa nchi vikiwemo vikosi vya jeshi.

Mwenendo wa kushindwa magaidi nchini Syria ni jambo ambalo limekuwa likiakisiwa pakubwa kimataifa. Aidha wigo wa jambo hilo umepanuka na kupiga hodi hadi katika vikao vya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa. Hapana shaka kuwa, matukio ya Syria kwa mara nyingine tena yameonyesha nafasi muhimu ya muqawama na kusimama kidete mbele ya njama mbalimbali zinazolikabili taifa fulani. Na hili ni jambo ambalo limeshuhudiwa katika hotuba ya Staffan de Mistura kuhusiana na matukio ya Syria na nafasi ya jeshi la nchi hiyo katika kuwashinda magaidi