UN yatahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya mvutano wa al-Aqsa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i32220-un_yatahadharisha_kuhusu_matokeo_mabaya_ya_mvutano_wa_al_aqsa
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu athari mbaya za mgogoro uliosababishwa na hatua ya Israel ya kuwazuia Waislamu wa Palestina kutekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa al Aqsa na kusisitiza kuwa, unaweza kuwa na maafa makubwa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 24, 2017 22:29 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya mvutano wa al-Aqsa

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu athari mbaya za mgogoro uliosababishwa na hatua ya Israel ya kuwazuia Waislamu wa Palestina kutekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa al Aqsa na kusisitiza kuwa, unaweza kuwa na maafa makubwa.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ya Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov amesema kuwa mgogoro wa sasa huko Quds unaweza kusababisha maafa makubwa zaidi ya kile kinachoshuhudiwa hivi sasa.

Askari wa Israel waliovamia Msikiti wa al Aqsa

Mladenov ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa jana wa Baraza la Usalama uliochunguza mgogoro wa sasa katika mji unaokaliwa kwa mabavu na Israel wa Quds, ametoa wito wa kukomeshwa mgogoro huo kabla ya Ijumaa ijayo. Amesema iwapo mgogoro huu utafika Ijumaa ijayo bila ya kupatia ufumbuzi unaweza kuwa na hatari kubwa katika medani.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa Mashariki ya Kati amesisitiza kuwa, japokuwa mgogoro wa sasa umetokeo katika mita kadhaa za Msikiti wa al Aqsa lakini athari zake mbaya zitakuwa na taathira kwa mamilioni bali mabilioni ya watu kote duniani. 

Wapalestina wakiswali nje ya Msikiti wa al Aqsa

Mgogoro wa sasa huko katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ulianza baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuliamuru jeshi la utawala huo haramu kufunga milango yote ya kuingia katika Msikiti wa al Aqsa na kuwazuia Waislamu kutekeza ibada ya Swala msikitini hapo. Hatua hiyo imezusha ghasia na machafuko makubwa katika ardhi za Palestina na inaendelea kulaaniwa na nchi na jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu.