Walowezi wa Kizayuni wauvamia msikiti wa al-Aqswa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i32644-walowezi_wa_kizayuni_wauvamia_msikiti_wa_al_aqswa
Makumi ya walowezi wa Kizayuni leo Alkhamisi wameuvamia tena msikiti wa al-Aqswa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu huko Baytul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2017 09:41 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wauvamia msikiti wa al-Aqswa

Makumi ya walowezi wa Kizayuni leo Alkhamisi wameuvamia tena msikiti wa al-Aqswa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu huko Baytul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Kwa mujibu wa Kanali ya Televisheni ya al-Alam, walowezi hao wa Kizayuni wameuvamia msikiti wa Aqswa kupitia lango la "Bab al Maghariba" wakiwa wamepewa ulinzi mkubwa na wanajeshi na maafisa usalama wa Israel na kuuvunjia tena heshima msikiti huo mtakatifu. 

Siku mbili zilizopita pia, mamia ya walowezi wa Kizayuni mara kadhaa wamevamia msikiti huo wa al-Aqswa na kuuvunjia heshima, hatua ambazo zimekabiliwa na malalamiko ya kila upande katika ulimwengu wa Kiislamu.

Wanajeshi wa Israel wakivamia msikiti wa al-Aqswa

Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Palestina aidha imesema, katika kipindi cha hivi karibuni, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameongeza kasi ya kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu ikiwa ni pamoja na kuongezeka njama za Tel Aviv za kuvuruga muundo wa kijamii, kihistoria na kidini wa mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas.

Hayo yanajiri huku mgogoro wa sasa huko katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ulioanza baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuliamuru jeshi la utawala huo haramu kufunga milango yote ya kuingia katika Msikiti wa al Aqswa na kuwazuia Waislamu kutekeza ibada ya Swala msikitini hapo ukiwa bado haujapoa. 

Itakumbukwa kuwa, Intifadha ya Tatu ya Wapalestina iliyoanza tarehe Mosi Oktoba 2015, ilianza baada ya wanajeshi na walowezi wa Kizayuni kuzidisha jeuri zao dhidi ya matukufu ya Kiislamu huko Palestina. Intifadha hiyo imepewa jina la Intifadha ya Masjidul Aqswa. Hadi hivi sasa zaidi ya Wapalestina 315 wameshauliwa shahidi na askari makatili wa Israel tangu ilipoanza Intifadha hiyo.