Jordan: Askari wa Kizayuni aliyeua Wajordan lazima ahukumiwe
Kufuatia mashinikizo na malalamiko ya Wajordan kuhusiana na kitendo cha askari wa utawala wa Kizayuni aliyeua raia wawili wa nchi hiyo, hatimaye serikali ya Amman imetangaza msimamo wake wa kutaka kupandishwa mahakamani askari huyo.
Msemaji wa serikali ya Jordan, Muhammad al-Mumin amesema kuwa, msimamo wa nchi hiyo kuhusiana na kadhia ya jinai ya mauaji iliyofanywa na afisa wa usalama wa ubalozi wa lsrael ambaye aliwaua raia wawili wa taifa hilo kwa kuwapiga risasi, ni suala lisilo na mjadala. Ameongeza kuwa, ikiwa lsrael itafungamana na suala hilo la kupandishwa kizimbani askari huyo, itasababisha taathira katika mahusiano ya pande mbili.
Kwa mujibu wa Muhammad al-Mumin, lsrael imeifahamisha serikali ya Amman kwamba maandalizi ya kimahakama yamekamilika kwa ajili ya kumpandisha kizimbani askari huyo na kwamba Jordan itaruhusiwa kufuatilia kwa karibu suala hilo. Siku chache zilizopita Ziff Moyal, askari wa Kizayuni aliyekuwa akilinda katika ubalozi wa utawala huo katili mjini Amman, aliwashambulia kwa kuwapiga risasi raia wawili wa Jordan waliokuwa karibu na ubalozi huo na kuwaua. Suala hilo liliibua hasira kali za Wajordan ambao mbali na kufanya maandamano makali waliitaka serikali ya nchi hiyo kufunga ubalozi wa utawala huo sambamba na kupandishwa kizimbani nchini mwao.
Mbali na raia wa kawaida kumiminika barabarani, makumi ya wabunge wa nchi hiyo ya Kiarabu walisusia vikao vya bunge, kulalamikia kitendo cha serikali ya Amman cha kumfungulia njia askari huyo muuaji na kuondoka ardhi ya Jordan. Malalamiko hayo yaliwafanya maafisa wote wa ubalozi huo akiwemo balozi mwenyewe wa lsrael kuondoka Jordan kwa kuogopa hasira za Wajordan.