Nguzo za msikiti mtukufu wa Al-Aqsa zinakaribia kuporomoka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33492-nguzo_za_msikiti_mtukufu_wa_al_aqsa_zinakaribia_kuporomoka
Taasisi ya Kimataifa ya Quds imetangaza kuwa nguzo za msingi wa msikiti wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu zinakaribia kuporomoka kutokana na mashimo na njia za chini ya ardhi zinazochimbwa kiholela na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 22, 2017 11:00 UTC
  • Nguzo za msikiti mtukufu wa Al-Aqsa zinakaribia kuporomoka

Taasisi ya Kimataifa ya Quds imetangaza kuwa nguzo za msingi wa msikiti wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu zinakaribia kuporomoka kutokana na mashimo na njia za chini ya ardhi zinazochimbwa kiholela na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika ripoti yake ya kila mwaka iliyotolewa leo, taasisi hiyo imetangaza kuwa idadi ya mashimo na njia za chini kwa chini zinazochimbwa na utawala ghasibu wa Kizayuni chini ya msikiti wa Al-Aqsa zimefikia 63 na kuna uwezekano nguzo za msingi wa msikiti huo zikaporomoka wakati wowote ule.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Taasisi ya Kimataifa ya Quds, kufanyika mwezi Mei mwaka huu kikao cha baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel katika moja ya njia za chini kwa chini katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa sambamba na kutimia miaka 50 tangu Quds tukufu kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu kikamilifu ni ujumbe wa wazi kwamba uchimbaji mashimo na njia hizo za chini kwa chini unaofanyika kwa usimamizi na uungaji mkono wa viongozi wa utawala huo haramu unalenga kueneza historia bandia na ya uongo ya Wazayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Mandhari ya mji wa Quds na msikiti wa Al-Aqsa

Ripoti hiyo imefafanua zaidi kwamba utawala wa Kizayuni umeshaidhinisha ujenzi wa hekalu katika eneo la Jabalul-Makbar, kusini magharibi ya eneo la kale la Quds na kwamba mradi wa treni ya angani katika eneo la karibu na msikiti mtukufu wa Al-Aqsa umepiga hatua kubwa.

Taasisi ya Kimataifa ya Quds imetoa indhari kuhusu maamuzi yanayochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuuzayunisha mji wa Baitul Muqaddas na kusisitiza kwamba hata eneo la makaburi yaliyoko kandokando ya msikiti wa Al-Aqsa hayajasalimika na hujuma za Wazayuni, ambapo utawala huo tayari umeshanyakua baadhi ya ardhi za makaburi hayo ili kuzibadilisha kwa kuwajengea bustani wazayuni katika siku za usoni.

Ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Quds imebainisha pia kuwa tangu mwezi Agosti 2016 hadi Agosti mwaka huu walowezi wa Kizayuni wapatao 23,661 wameuvamia na kuuvunjia heshima msikiti mtukufu wa Al-Aqsa, likiwa ni ongezeko la asilimia 58 la vitendo hivyo kulinganisha na mwaka uliopita.

Walowezi wa Kizayuni wakiingia kwenye msikiti wa Al-Aqsa ili kukivunjia heshima kibla cha kwanza cha Waislamu

Msikiti wa Al-Aqsa ambao ni nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina iliyoko kwenye mji wa Baitul Muqaddas umekuwa kila mara ukiandamwa na hujuma za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel za kuubomoa msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.../