Ansarullah: Wananchi wa Yemen hawana imani na Umoja wa Mataifa
Msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameukosoa utendaji wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na jinai zinazofanywa na utawala wa Aal Saud na kusisitiza kuwa wananchi wa Yemen hawana imani na umoja huo.
Muhammad Abdussalam ametoa msimamo huo katika jibu na radiamali kwa jinai za hivi karibuni zilizofanywa na utawala wa Saudia na waitifaki wake katika mji mkuu wa Yemen Sana'a na kuongeza kuwa: Umoja wa Mataifa unabeba dhima ya kuendelea kuuawa raia wa Yemen kutokana na kupuuza jinai zinazofanywa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud.
Ndege za kivita za Saudia, siku ya Jumatano ziliua kwa umati raia wasiopungua 60 na kuwajeruhi na makumi ya wengine katika shambulio zililofanya katika wilaya ya Arhab kwenye mji mkuu wa Yemen, Sana'a.

Msemaji wa harakati ya Ansarullah amebainisha kuwa Umoja wa Mataifa hauna nia ya dhati ya kuitisha uchunguzi kuhusu jinai zinazofanywa na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia na Marekani na mtu hawezi kujenga matumaini kwa taasisi hiyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo watu wasiopungua 14 wakiwemo wanawake wawili na watoto wadogo sita waliuawa hapo jana katika shambulio jengine lililofanywa na ndege za kivita za muungano vamizi unaoongozwa na Saudia katika mji wa Attan jirani na mji mkuu wa Yemen Sana'a.

Mashambulio ya anga yanayofanywa mtawalia usiku na mchana na ndege za kivita za Saudi Arabia nchini Yemen yameshaua watu zaidi ya 12,000 hadi sasa, wakiwemo wanawake na watoto na kuwafanya wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makaazi tangu utawala huo wa Aal Saud ulipoanzisha vita dhidi ya nchi hiyo mwezi Machi mwaka 2015 kwa madhumuni ya kuisambaratisha harakati ya wananchi ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abd Rabbuh Mansur Hadi.../