Rais Erdoğan: Kupeperushwa bendera ya Israel Kurdistan, hakutawaokoa watu wake
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametoa radiamali kufuatia kupeperushwa bendera ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndani ya eneo la Kurdistan la Iraq lililofanya kura ya maoni Jumatatu iliyopita.
Rais Erdoğan aliyasema hayo katika sherehe za kuanza mwaka mpya wa masomo mjini Ankara ambapo sambamba na kulalamikia kura ya maoni iliyofanyika siku ya Jumatatu kwa ajili ya kutaka kujitangazia uhuru na kujitenga na serikali kuu ya Iraq, amesema kuwa, kupeperushwa bendera ya Israel ndani ya eneo hilo lenye mamlaka ya ndani, hakutawaokoa raia na viongozi wake.
Akisisitiza kuwa, Uturuki imeweka mezani machaguo ya kiuchumi na kijeshi kwa ajili ya kuikabili Kurdistan, amewataka viongozi wa eneo hilo kuachana na njia ya kujitenga ambayo ameitaja kuwa isiyo na natija yoyote ghairi ya giza tupu. Kadhalika Rais Erdoğan ameashiria kura ya maoni ya Jumatatu iliyopita na kusema kuwa, kufanyika kwa kura hiyo kumejiri kinyume cha sheria na kwamba mbali na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel hakuna nchi wala taasisi nyingine iliyoitambua kura hiyo. Kabla ya hapo Rais Erdoğan alitoa onyo kali akisema kuwa, ikiwa viongozi wa eneo la Kurdistan wataendelea kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, basi Ankara italazimika kuliwekea vikwazo eneo hilo sambamba na kutekeleza chaguo la kijeshi dhidi yao.
Mbali na Uturuki, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq na Syria zimelaani kura hiyo ya maoni ya kutaka kujitenga eneo hilo la Kurdistan ambapo pia zimetoa onyo kali kwa Masoud Barzani, kiongozi mkuu wa eneo hilo juu ya hatua yake hiyo. Hata hivyo licha ya indhari hizo, Jumatatu ya tarehe 25 mwezi huu, serikali ya eneo hilo ilifanya kura hiyo ya maoni sambamba na kuwalazimisha wakazi wake kushiriki.