Saudia yapongeza vikwazo vya Marekani dhidi ya Hizbullah, nayo Hizbullah yaonya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i35443-saudia_yapongeza_vikwazo_vya_marekani_dhidi_ya_hizbullah_nayo_hizbullah_yaonya
Waziri Mshauri wa Saudi Arabia katika Masuala ya nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi, amepongeza vikwazo vya serikali ya Marekani dhidi ya harakati ya Kiislamu ya muqawama Hizbullah nchini Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2017 11:42 UTC
  • Saudia yapongeza vikwazo vya Marekani dhidi ya Hizbullah, nayo Hizbullah yaonya

Waziri Mshauri wa Saudi Arabia katika Masuala ya nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi, amepongeza vikwazo vya serikali ya Marekani dhidi ya harakati ya Kiislamu ya muqawama Hizbullah nchini Lebanon.

Thamer Al-Sabhan amedai kuwa vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Hizbullah ni vizuri na kuongeza kuwa, pamoja na hayo njia bora ya kukabiliana na harakati hiyo ya Kiislamu ni kuundwa muungano wa kimataifa dhidi ya Hizbullah na washirika wake. Katika matamshi hayo ambayo yanafanana na yale yaliyotolewa na utawala haramu wa Israel na makundi ya kigaidi, Thamer Al-Sabhan amedai kuwa, kupambana na Hizbullah ni kwa ajili ya kurejesha usalama na amani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah

Itakumbukwa kuwa tarehe 28 Septemba mwaka huu, kamati ya mahusiano ya kigeni ya Kongresi ya Marekani ilipitisha muswada wa kushadidishwa vikwazo dhidi ya harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon. Muswada huo utawasilishwa hivi karibuni katika Seneti ya nchi hiyo kwa ajili ya kupigiwa kura na maseneta ambapo ikiwa utapitishwa utapelekwa kwa Rais Donald Trump wa nchi hiyo ili autie saini kuwa sheria. Hayo yanajiri katika hali ambayo, harakati hiyo ya Kiislamu ya Hizbullah imekuwa na nafasi athirifu katika vita dhidi ya magaidi, kuzuia njama za Marekani, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Saudia katika eneo la Mashariki ya Kati, suala ambalo limezichukiza mno serikali za Washington, Tel Aviv na Riyadh.

Mmoja wa makomando wa harakati ya Hizbullah

Wakati huo huo, mjumbe wa baraza kuu la harakati ya Hizbullah nchini Lebanon, Sheikh Nabil Qaouk amesema kuwa uingiliaji wa Saudia katika masuala ya ndani ya Lebanon ni kengele ya hatari sana kwa nchi hiyo. Amesisitiza kuwa nchi ambayo inaitakia Lebanon kheri, haiwezi kuwa mchochezi wa kuibua vita ndani ya taifa hilo. Sheikh Nabil Qaouk amesema kuwa hivi sasa uingiliaji wa Saudia katika masuala ya ndani ya Lebanon umekuwa dhahiri na kwamba hatua ya Walebanon wengi kuendelea kushikamana na misingi ya umoja wa kitaifa, imeifedhehesha Riyadh na washirika wake.