Amir wa Qatar awaonya wanaofanya njama za kuishambulia kijeshi nchi yake
Amir wa Qatar, Tamim Bin Hamad al-Thani ameonya kuwa, hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi italitumbukiza eneo zima la Mashariki ya Kati katika machafuko.
Sheikh Tamim ametoa indhari hiyo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Marekani ya CBS ambayo yatarushwa hewani leo usiku na kusisitiza kuwa: "Nina wasi wasi iwapo chochote kitafanyika, iwapo hatua yoyote ya kijeshi itachukuliwa, eneo hili litatumbukia katika ghasia."
Kadhalika ameashiria kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani alitoa pendekezo la kuwa mpatanishi wa mgogoro uliopo huko Camp David, lakini Saudia na waitifaki wake hawajatoa jibu lolote kuhusu pendekezo hilo hadi sasa.
Hii ni katika hali ambayo, wiki mbili zilizopita, Abdullah bin Hamad al-Attiyah, Naibu Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar aliliambia gazeti la Uhispania la ABC kuwa, Imarati ilikodisha kampuni binafsi ya usalama ya Marekani iliyojulikana kama "Blackwater-linked" ambayo kwa sasa inafahamika kama Academi, kwa lengo la kuwapa mafunzo mamluki ambao wangetumwa katika operesheni ya kijeshi ya kuivamia Qatar.
Ifahamike kuwa, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri tarehe 5 Juni mwaka huu zilitangaza kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi, madai ambayo yamekabidhibishwa vikali na serikali ya Doha.
Kwengineko kwenye mahojiano hayo, Amir wa Qatar, Tamim Bin Hamad al-Thani amebainisha kuwa, vikwazo na mzingiro wa Saudia na waitifaki wake vimelenga uhuru wa Qatar na kwaba uhuru wa kujitawala Qatar ni mstari mwekundu wa nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.