UN: Saudia inazuia kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa Wayemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36218-un_saudia_inazuia_kufikishwa_misaada_ya_kibinadamu_kwa_wayemen
Umoja wa Mataifa umesema hatua ya Saudi Arabia kufunga mipaka ya ardhini, angani na baharini ya Yemen imepelekea umoja huo ushindwe kufikisha misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wanaosumbuliwa na njaa wa nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 07, 2017 04:46 UTC
  • UN: Saudia inazuia kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa Wayemen

Umoja wa Mataifa umesema hatua ya Saudi Arabia kufunga mipaka ya ardhini, angani na baharini ya Yemen imepelekea umoja huo ushindwe kufikisha misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wanaosumbuliwa na njaa wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Msemaji wa UN, Farhan Haq amesema walitazamia kutuma ndege mbili zenye shehena za chakula na bidhaa nyingine muhimu kwa ajili ya mamilioni ya Wayemen hapo jana lakini hilo likashindikana kutokana na kitendo hicho cha Saudia.

Amesema kwa sasa umoja huo unafanya jitihada za kuishawishi Saudia ikubali kutumwa misaada hiyo ya kibinadamu ili kunusuru maisha ya raia zaidi ya milioni 7 wa Yemen wanaosumbuliwa na utapiamlo.

Farhan Haq, Msemaji wa UN

Siku ya Jumapili, utawala wa Aal-Saud ulitangaza kufunga mipaka yote ya angani, ardhini na baharini ya Yemen, baada ya vikosi vya wananchi vya kujitolea vya Ansarullah kulenga kwa kombora la balestiki uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mfalme Khalid ulioko kwenye mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh. 

Vita vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen vilianzishwa mwezi Machi mwaka 2015 kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi.

Watu zaidi ya 13,000 , wengi wakiwa ni wanawake na watoto, wameuawa katika hujuma ya Saudia nchini Yemen.