Licha ya kutakiwa arudi Lebanon, Saad Hariri ashindwa kufanya hivyo
Licha ya viongozi mbalimbali wa Lebanon kumtaka Saad Hariri, Waziri Mkuu wa nchi hiyo aliyejiuzulu wadhifa wake, arejee nchini kutoka Saudia, vyombo vya habari vimetangaza leo kwamba Hariri ameshindwa kufanya hivyo na badala yake amerejea mlinzi wake pekee Bairut, mji mkuu wa nchi hiyo.
Picha zilizochukuliwa katika uwanja wa ndege wa Mfalme Khalid wa mjini Riyadh, zimemuonyesha Mohammad Diab, mlinzi maalumu wa Hariri akirejea peke yake kutoka Saudia kwenda Lebanon. Awali Saudia ilimwalika Hariri nchini humo bila kuandamana na washauri wake ambapo aliwasili Riyadh akiwa na walinzi wawili pekee.
Wakati huo huo, Adel al-Jubeir Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia sambamba na kujibu baadhi ya habari zinazosema kuwa Saad Hariri amewekwa kizuizi mjini Riyadh, amedai kuwa Saudia haikumlazimisha kiongozi huyo kujizulu washifa wake huo na kwamba yuko huru nchini Saudia. Kadhalika al-Jubeir aliongeza kuwa, wakati wowote Hariri atakapotaka kurejea nchini kwake basi atafanya hivyo.
Hii ni katika hali ambayo wanasiasa mbalimbali nchini Lebanon akiwemo Adnan Mansour, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo wamethibitisha kwamba, kujiuzulu Hariri huko Saudia kulifanyika kwa mashinikizo ya utawala wa Aal-Saud hasa kwa kuzingatia kuwa, ushindi wa muqawama nchini Iraq na Syria umezikasirisha mno Marekani, Israel na baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati. Aidha hatua ya Hariri ya kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah, ni takwa kuu la Riyadh ili kufikia malengo yake machafu katika eneo.