Mkenya apigwa risasi na jirani mbaguzi nchini Marekani, polisi walaaniwa kwa kushindwa kuchukua hatua
Polisi huko Minneapolis, jimbo la Minnesota, Marekani, hatimaye wamemkamata mzungu mbabuzi, wiki moja baada ya kumpiga risasi na kumjeruhi jirani yake mwenye asili ya Kenya, kwa kile kinachoaminika kuwa ni hujuma ya ubaguzi wa rangi na chuki.
Davis Moturi alikuwa akikata miti nje ya boma lake wakati jirani yake, John Sawchak, alipompiga risasi shingoni katika kisa cha jaribio la mauaji.
Katika video zinazosambaa mtandaoni, Moturi alionekana akianguka chini, huku mashine yake ya kukata miti ikiendelea kuzunguka kando yake.
Polisi huko Minneapolis wamelaaniwa vikali baada ya kuchukua zaidi ya wiki moja kumkamata mshukiwa, na baada ya kushindwa kuchukua hatua wakati Moturi aliripoti Sawchak kwa polisi mara 20 kwa unyanyasaji ambao hatimaye uliishia kwa kupigwa risasi.
Mkuu wa Polisi wa Minneapolis Brian O'Hara alikiri kwamba polisi walifeli kumsaidia Moturi kwa wakati, huku akielezea hatua walizochukua ili kumkamata mshukiwa, ambaye amefunguliwa mashtaka ya jaribio la mauaji na ubaguzi wa rangi.
Marekani daima huwa katika vichwa vya habari duniani kote kutokana na mashambulizi ya ubaguzi wa rangi ambapo watu weusi au wenye asili ya Afrika wanalalamika sana kuhusu ubaguzi wa kitaasisi dhidi yao.
Kulingana na data ya Kituo cha Utafiti cha Pew, takriban Waafrika wenye asili ya Amerika wanane kati ya 10 wanasema wamekumbana na ubaguzi kwa sababu ya rangi zao. Mashambulizi hayo aghalabu hutekelezwa na wazungu wabaguzi wenye misimamo mikali ya chuki.