Kusambaratishwa ISIS mashariki mwa Syria
Hatua ya wanajeshi wa Syria na waitifaki wao ya kuingia katika mji wa mpakani wa al-Bukamal ina maana ya kusambaratishwa kikamilifu magaidi wa Daesh (ISIS) mashariki mwa nchi hiyo. Mafanikio hayo makubwa yaliyopatikana katika vita dhidi ya ugaidi yamekuja wiki moja baada ya kukombolewa mji wa kiistratijia wa Deir ez-Zor kutoka katika makucha ya magaidi wa ISIS wanaoungwa mkono na madola ya kigeni ukiwemo utawala wa Kizayuni wa Israel.
Itakumbukwa kuwa Ijumaa iliyopita yaani tarehe 3 Novemba, komandi ya jeshi na vikosi vya ulinzi vya Syria ilitangaza rasmi kukombolea kikamilifu mji wa Deir ez-Zor kutoka mikononi mwa Daesh na kusisitiza kwamba jeshi la Syria litaendelea na mapambano yake hadi litakapowasafisha kikamilifu magaidi nchini humo. Wakati huo huo televisheni ya al Mayadeen ya nchini Lebanon Jumatano usiku ilitangaza kuwa jeshi la Syria kwa kushirikiana na vikosi vya muqawama limefanikiwa kuukomboa pia mji wa al-Bukamal ambao unahesabiwa kuwa ngome ya mwisho ya magaidi wa Daesh kusini mwa mkoa wa Deir ez-Zor. Mji huo wa mpakani unapakana na mji wa al Qaima wa Iraq ambao nao tarehe 3 Novemba ulikombolewa na vikosi vya ulinzi vya Iraq, suala ambalo limerahisisha kukombolewa pia mji wa al-Bukamal wa Syria katika upande wa pili wa mpaka wa nchi hizo mbili.
Ushindi wa haraka sana wa jeshi la Syria na waitifaki wake huko mashariki mwa Syria umepelekea kukaribia mno kufungwa faili la magaidi wa ISIS nchini humo ambapo hivi sasa wameshapoteza maeneo na ngome zao zote isipokuwa baadhi ya maeneo ya jangwani na ya pambizoni mwa mikoa ya Deir ez-Zor na Homs. Amma uhakika huu haupingiki kwamba kuangamizwa magaidi wa Daesh nchini Syria kuna maana ya kushindwa maadui wa nchi hiyo ambao walikusudia kufanya njama kubwa na za miaka mingi kwa kutumia magaidi wa ISIS.
Kusambaratika kwa mkupuo mmoja genge la kigaidi la Daesh katika nchi za Syria na Iraq kuna ujumbe muhimu wa kiistratijia nao ni kwamba, ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Syria na Iraq pamoja na Russia umesambaratisha njama za waungaji mkono wa magaidi wa ISIS katika eneo hili kiasi kwamba leo hii tena hakuna yeyote anayezungumzia "Khilafa" bandia iliyodaiwa kuundwa na Daesh katika ardhi za Iraq na Syria. Mafanikio hayo ni matunda ya mapambano ya ikhlasi na ya kweli dhidi ya ugaidi na kwamba nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mafanikio hayo iko wazi kabisa. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo hiyo ndio maana Ali Akbar Velayati, mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa akasema siku ya Jumanne usiku huko Halab Syria kwamba: Matunda ya ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na muqawama katika nchi za Syria na Iraq ni kushindwa njama za maadui wanaoutakia mabaya ulimwengu wa Kiislamu.
Naam, mshale wa mwisho ulioimaliza na kuikata roho Daesh ni huko kukombolewa mji wa kiistratijia na muhimu sana wa mpakani yaani mji wa al Bukamal. Mafanikio hayo ya jeshi la Syria na waitifaki wake yamebadilisha upepo wa matukio kwa faida ya kambi ya muqawama wa Kiislamu na kwa madhara ya nchi kama Saudia na Marekani pamoja na utawala pandikizi wa Kizayuni wa Israel ambao ndio waanzilishi na waungaji mkono wakubwa wa magenge ya kigaidi nchini Syria. Amma uhakika huu nao ni muhimu kuutaja hapa kwamba kuchomwa moto na kuangamizwa kikamilifu zimwi la Daesh nchini Syria na Iraq kumetokana na mwamko na umakini wa wananchi wa nchi hizo mbili ambao mara zote wako pamoja na vikosi vyao vya ulinzi licha ya kubebeshwa masaibu na hasara kubwa na kamwe hawakuruhusu kufanikiwa njama za maadui dhidi ya nchi huru za Kiislamu. Fauka ya hayo ni kwamba, hali ilivyo hivi sasa katika medani za mapambano huko Syria na Iraq inaonesha kuwa, kambi ya muqawama inayoundwa na Iran, Iraq, Syria na Lebanon kwa kushirikiana na Russia ni kizuizi kikubwa kilichosambaratisha njama za magaidi; na ushahidi wa hayo unaonekana wazi katika matukio ya hivi karibuni ya Syria na Iraq kama vile kufurushwa magaidi wa Daesh na kukombolewa miji mwili muhimu ya kiistratijia inayozitenganisha nchi hizo mbili yaani al Bukamal upande wa Syria na al Qaim upande wa Iraq.