Uchezaji kamari hatari wa Riyadh kwa kutumia turufu iliyopikuliwa ya Israel
Kitendawili cha matukio ya eneo la Mashariki ya Kati kimeanza kutatuliwa pole pole baada ya kukaribia kukamilika utegaji wa kitendawili hicho.
Ufumbaji wa fumbo hilo umeanza kukamilika baada ya pande mbili, Riyadh na Tel Aviv kutoa vitisho vya wazi vya kijeshi dhidi ya Lebanon lakini hapo hapo zikapata majibu makali kutoka kwa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbulla ambaye hakuzungumzia suala hilo kwa njia uchambuzi, bali amejibu kwa sura ya habari na taarifa kwamba ukoo wa Aal Saud wa Saudi Arabia unatumia turufu iliyopikuliwa ya Wazayuni kutaka kufanya mashambulizi mapya dhidi ya Lebanon.

Uteguaji wa kitendawili hicho ulifanywa na Sayyid Hassan Nasrullah siku ya Ijumaa wakati alipotoa hotuba muhimu kwa mnasaba wa Siku ya Shahidi na kusisitiza kuwa, uvamizi wowote unaoweza kufanywa na Israel dhidi ya Lebanon si mpango uliopangwa na Tel Aviv, bali ni njama za Saudi Arabia.
Matokeo ya muungano wa Kiebrania-Kiarabu ambao uligunduliwa mwaka jana baada ya kufichuka mazungumzo ya siri baina ya viongozi wa Saudia na wa utawala wa Kizayuni wa Israel na ambayo yalipata nguvu zaidi wakati wa mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 na hatimaye yakashindwa kuzaa matunda, hivi sasa muungano huo umegeuka kuwa umoja wa kijeshi dhidi ya nchi za Kiislamu. Saudi Arabia ambayo inadai kuwa ni mkuu wa ulimwengu wa Kiislamu inaomba msaada wa Wazayuni kuwasha moto mpya wa vita katika eneo hili na ina nia ya kutumia dola zake za mafuta zilizojaa damu kuendesha opesheni ya kijeshi ya Wazayuni dhidi ya Lebanon.
Tab'an, kabla ya hapo, utawala wa Kizayuni wa Israel umepata pigo mara chungu nzima huko Lebanon na una kumbukumbu chungu kuhusu uingiliaji wake wa mambo ya ndani ya Lebanon. Pamoja na hayo si jambo lililo mbali kwa Saudi Arabia kuzusha vita vipya katika eneo hili kwa nia ya kuichokoza Iran ili kwa njia hiyo iweze kwa mara nyingine kujaribisha bahati yake katika vita vya pande zote ilivyovitangaza dhidi ya kambi ya muqawama wa Kiislamu.
Matamshi ya hivi karibuni ya Adel al Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia aliyesema kuwa ni matumaini yetu hatutoingia katika vita vya ana kwa ana na Iran yanaonesha kuwa shabaha kuu ya muungano wa Kiebrania-Kiarabu ya kutaka kuwasha moto wa vita katika eneo hili si Lebanon, bali ni Iran.

Mafanikio makubwa yaliyopatikana katika vita dhidi ya ugaidi kwenye eneo hili ikiwa ni pamoja na kuangamizwa magaidi wa Daesh (ISIS) katika nchi za Iraq na Syria na vilevile "mashaya" na matembezi makubwa ya Arubaini ya Imam Husain AS ambayo yameonesha nguvu laini za Iran zinazowavutia Waislamu wa madhehebu yote, ni mambo ambayo yameutia wahka na wasiwasi mkubwa ukoo wa Aal Saud.
Si hayo tu, lakini pia, Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia hivi sasa anataka kuubadilisha muundo wa kisiasa wa nchi hiyo uwe kwa namna ambayo utamfanya awe dikteta asiye na mpinzani nchini humo na ndio maana amewatia mbaroni wanawafalme wote wanaompinga na ambao wanaonekana ni tishio kwake. Hivyo hali ya kisiasa ndani ya Saudia hivi sasa ni ya mzozo. Nchi hiyo inahitajia zaidi umoja baina ya wanawafalme na kunatakiwa kufanyike juhudi za ziada za kuondoa vinyongo vinavyotokana na kutiwa mbaroni wana wa wafalme wa nchi hiyo. Sasa badala ya viongozi wanagenzi wa Saudia kufikiria njia sahihi za kuleta umoja huo, wanadhani kwamba wakianzisha vita vipya wataweza kurejesha mshikamano wa ndani ya Saudia. Lakini vita hivyo lazima viwe dhidi ya nchi muhimu kama Iran ambavyo vitaweza kuchochea hisia za watu ndani ya Saudia na kuwasahaulisha ukandamizaji na udikteta wa bin Salman.
Sababu hizo mbili ukiongeza juu yake uchochezi wa Marekani zinaonekana umewapandisha kiburi watawala wa Riyadh na kuwafanya watoe ujumbe kwa Tehran kwamba wako tayari kukabiliana nayo kijeshi.

Ni jambo lililo wazi kwamba busara za Tehran hazitoiruhusu ijitumbukize kwenye mchezo huo wa kitoto. Iran ni mtetezi mkuu wa umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu na inaamini kuwa, nguvu na uwezo wote wa nchi za Kiislamu unapaswa utumike kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel na si baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe.
Muhimu zaidi ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewanyooshea mkono wa urafiki na mapenzi Waislamu wote bila ya kujali madhehebu yao. Ni hivi karibunu tu Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilituma ujumbe wake muhimu hapa Tehran na kufanya mazungumzo na viongozi wa Iran. Uhusiano mzuri baina ya Tehran na Hizbullah ya Lebanon nao uko wazi.
Lakini pia tusiisahau nukta hii iliyogusiwa na Mohsen Rezai, Katibu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliposema: Uvamizi wa pamoja wa Saudia na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon unaweza kulitumbukiza katika moto eneo hili zima na kwamba lawama za kosa hilo la kiistratijia zitauendea ukoo wa Aal Saud iwapo utakuwa tayari kucheza kamari hiyo ya kipumbavu.