Iraq: Kiongozi wa Daesh yuko hai, anaishi kwa kujificha kama mapanya
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iraq amefichua kwamba, ripoti za kiintelijensia zinaonesha kwamba, kiongozi wa kundi la kigaidi na kiwahabi la Daesh, Abu Bakr al Baghdadi bado yuko hai na anajificha katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Syria.
Jenerali Yahya Rasul amesema kuwa, taarifa za kipelelezi zinathibitisha kuwa al Baghdadi yuko hai na anaishi kwa kuhamahama katika maeneo ya jangwani katika mpaka wa Iraq na Syria. Amesema eneo hilo lingali na wapigajani wa kundi la Daesh wanaokadiriwa kufikia makumi kadhaa.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iraq amesisitiza kuwa, kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh anaishi kwa kuhamahama baina ya wapiganaji hao na kujificha kwenye mashimo kama mapanya kandokando ya mto Furati. Amesema baadhi ya wapiganaji wa kundi hilo wanajificha katika mavazi ya wakulima wa maeneo yaliyoko baina ya mji wa al Qaim na al Bukamal.
Baadhi ya habari zinasema Abu Bakr al Baghdadi analindwa na maafisa wa jeshi la Marekani na kwamba Washington haitamuua au kumtia nguvuni ila iwapo italazimika kufanya hivyo.