Uturuki: Baadhi ya nchi za Kiarabu zinaiogopa mno Marekani
Uturuki imekosoa kile ilichokieleza kama hatua na msimamo dhaifu wa nchi za Kiarabu kuhusiana na uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuitambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Uturuki imetoa kauli hiyo wakati nchi hiyo inatazamiwa kuongoza kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kinachotazamiwa kufanyika leo mjini Istanbul kujadili uamuzi huo wa Trump ambao umelaaniwa na kukosolewa vikali katika kila pembe ya dunia.
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ambaye amemtuhumu Rais wa Marekani kuwa amepuuza madai ya Wapalestina kuhusiana na Baitul Muqaddas Mashariki na "kukanyaga sheria za kimataifa", amewaalika viongozi wa nchi zaidi ya 50 za Kiislamu kwenye kikao maalumu kwa ajili ya kuchukua msimamo juu ya suala hilo. Erdogan aidha amesema Rais wa Marekani ni mshirika wa umwagaji damu utakaotokea kutokana na uamuzi aliochukua.
Kutokana na hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kutotangaza rasmi kama zitashiriki au zitatuma ujumbe gani katika kikao cha leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema: "baadhi ya nchi za Kiarabu zimeonyesha msimamo dhaifu mno". Cavusoglu ameongeza kuwa: "Inavyoonekana, baadhi ya nchi zinaiogopa mno Marekani".
Inafaa kuashiria kuwa Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zimetangaza kuwa zitawakilishwa na mawaziri wa mambo ya nje katika kikao cha leo cha OIC, wakati hadi jana usiku Saudi Arabia ilikuwa bado haijatngaza kama itashiriki kwenye kikao hicho.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawakilishwa na Rais Hassan Rouhani katika kikao hicho cha dharura cha OIC.
Hayo yanajiri huku viongozi wa Palestina wakitoa wito kwa kikao cha dharura cha OIC kuitambua rasmi Baitul Muqaddas Mashariki kuwa mji mkuu wa Palestina.../