Dec 23, 2017 15:23 UTC
  • Ismail Haniya: Quds Tukufu iliyoungana ni mji Mkuu wa Palestina

Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Ismail Haniya amesema, mji wa Quds (Jerusalem) ulioungana ni mji mkuu wa nchi huru ya Palestina, na nchi za Kiislamu na Kiarabu hazitaipuuza Quds.

Haniya ameyasema hayo leo katika Mkutano wa 11 wa Kimataifa wa Quds katika mji wa Ghaza. Ameongeza kuwa, kile ambacho kinajiri leo Palestina si Intifadha au mwamko tu bali ni Intifadha ya dunia nzima dhidi ya adui. Amesema ni kwa msingi huo ndio maana aghlabu ya nchi za dunia zikabainisha mtazamo wao katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kupinga hatua ya Marekani ya kutambua Quds kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Haniya ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Hamas ameendelea kusema kuwa, Quds ni nembo ya kidini ya Palestina na kwa msingi huo kuna vita vigumu baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuulinda mji huo. Amesema Wazayuni wanatekeleza njama za kuibua nembo bandia za kidini na kihistoria katika Quds Tukufu ili hatimaye wanyakue kikamilifu mji huo.

Msikiti wa Al Aqsa

Kiongozi huyo wa Hamas amesisitiza kuwa, Quds ni mji mkuu wa kisiasa wa taifa la Palestina na pia ni mji mkuu wa kidini wa Waislamu wote duniani. Halikadhalika amesema Quds ni mji mkuu wa wanadamu, maadili, thamani zawapemdao uhuru wote, wawe ni Waislamu au Wakristo. Halikadhalika amesema Wapalestina hawatafanya mazungumzo kuhusu hatima ya Quds.

Ismail Haniya amesema, hii leo watu wa Palestina wanapaswa kuchukua maamuzi imara ya kuvunja njama za Marekani.

Disemba sita Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa eti Quds ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, hatua ambayo imepingwa na ghlabu ya nchi duniani.

Tags