Émile Lahoud: Iran na Hizbullah zimeifanya Israel ichanganyikiwe
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i38259-Émile_lahoud_iran_na_hizbullah_zimeifanya_israel_ichanganyikiwe
Rais wa zamani wa Lebanon, Émile Lahoud amesema kuwa nafasi na mchango muhimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na harakati ya Hizbullah ya Lebanon vimeifanya Israel ichanganyikiwe sambamba na kuharibikiwa mahesabu yake yote katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2017 12:13 UTC
  • Émile Lahoud: Iran na Hizbullah zimeifanya Israel ichanganyikiwe

Rais wa zamani wa Lebanon, Émile Lahoud amesema kuwa nafasi na mchango muhimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na harakati ya Hizbullah ya Lebanon vimeifanya Israel ichanganyikiwe sambamba na kuharibikiwa mahesabu yake yote katika eneo la Mashariki ya Kati.

Lahoud ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na kanali ya televisheni ya kimataifa ya al-Kauthar na kusisitiza kwamba, hotuba ya hivi karibuni ya Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah juu ya kwenda Palestina mamilioni ya wanamuqawama kwa ajili ya kuitetea Quds, (Jerusalem) na kadhalika uungaji mkono wa Qasem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kwa hatua hiyo, vimeutia kiwewe utawala haramu wa Israel sambamba na kulazimika kuangalia upya mahesabu yake.

Rais wa zamani wa Lebanon, Émile Lahoud

Rais wa zamani wa Lebanon amesema, kulazimika kurudi nyuma Israel kutoka katika mipaka ya kusini mwa Lebanon hapo mwaka 2000 na kadhalika kushindwa vibaya utawala huo kwa kipigo cha wanamapambano wa Hizbullah katika vita vya siku 33 kipindi cha msimu wa joto mwaka 2006, kuliithibitishia dunia kwamba, wakati wowote kundi fulani linapoamua kusimama kidete kwa kutumia imani yake, basi linaweza kumshinda adui hata kama adui huyo atakuwa na nguvu kiasi gani.

Akieashiria sababu ya yeye kupinga vikali pendekezo la kutaka kunyang'anywa silaha harakati ya Hizbullah, Émile Lahoud amesema kuwa sio rahisi kuulenga moja kwa moja muqawama kwa kuwa ni mithili ya jeshi ambalo halina mahala maalumu na kwamba silaha za Hizbullah zinatakiwa kuendelea kuwa mkononi mwa harakati hiyo kwani hatua hiyo inakamilisha uwezo wa jeshi la Lebanon.

Kiongozi Muadhamu Sayyid Ali Khamenei kulia, Sayyid Hassan Nasrullah katikati na Qasem Soleimani mwishoni

Kadhalika rais wa zamani wa Lebanon ameashiria maamuzi ya hivi karibuni ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ya kuliweka jina la harakati ya Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi na kusisitiza kuwa, hatua hiyo si tu kwamba haiwezi kuidhoofisha nafasi ya Hizbullah ndani ya nchi za Kiarabu, bali ndio kwanza imeifanya kuwa imara zaidi.

Katika sehemu nyingine Émile Lahoud ameashiria hatua ya kijuba ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa kuutangaza mji wa Quds kuwa mji mkuu wa Israel na kusema, Quds ni mali ya Waislamu na Wakristo na kamwe hauwezi kuwa mji wa Israel.