UAE iliilipa kampuni ya Marekani kueneza propaganda dhidi ya Qatar
(last modified Sun, 21 Jan 2018 07:48:07 GMT )
Jan 21, 2018 07:48 UTC
  • UAE iliilipa kampuni ya Marekani kueneza propaganda dhidi ya Qatar

Shirika la habari la NBC News limefichua kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu uliilipa kampuni moja ya Marekani dola 333,000 ili kueneza propaganda chafu dhidi ya Qatar mwaka jana.

Kampuni ya SCL Social Limited imethibitisha kuwa ilipokea fedha hizo mwaka jana kutoka Baraza la Vyombo vya Habari la Imarati kwa ajili ya kueneza propaganda dhidi ya Qatar katika mitandao ya kijamii. 

Kampuni hiyo ilisambaza habari, matangazo ya biashara na hata picha za upotoshaji zinazoonyesha kuwa Doha inaunga mkono ugaidi.

Habari zinasema kuwa, kampuni hiyo ya Marekani ilichapisha matangazo ya biashara yaliyokuwa hasi dhidi ya Qatar katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na YouTube, Septemba mwaka jana wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mji wa Doha, Qatar

Juni mwaka jana, Saudi Arabia, Imarati, Misri na Bahrain zilichukua hatua mbalimbali za uhasama dhidi ya Qatar kwa lengo la kuishinikiza serikali ya Doha kutii matakwa yao. 

Mbali na kukata mahusiano yote ya kidiplomasia na Qatar, nchi hizo pia ziliiwekea mzingiro Doha katika pande zote za ardhini, angani na baharini.

 

Tags