Jeshi la Syria lajibu mapigo, latungua makombora ya Israel
Jeshi la Syria limetoa jibu kali kwa uvamizi mpya wa Israel, baada ya utawala huo wa Kizayuni kuanzisha mashambulizi ya makombora viungani mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus.
Kanali ya televisheni ya al-Ikhbaria ya Syria imesema mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi hiyo umetungua makombora ya Israel, yaliyovurumishwa kulenga kituo cha utafiti wa kisayansi katika kijiji cha Jamraya, nje kidogo ya Damascus mapema leo Jumatano.
Katika miaka ya hivi karibuni, utawala haramu wa Israel umekuwa ukitekeleza mashambulizi yanayolenga vituo vya kijeshi vya Syria, kwa kisingizio cha kupambana na magenge ya kigaidi, lakini umekuwa ukikabiliwa na jibu kali.
Hii ni katika hali ambayo, mbali na Tel Aviv kuyapa silaha makundi ya kigaidi yanayopambana na serikali halali ya Damascus, lakini pia imekuwa ikiwapa matibabu matakfiri waliojeruhiwa nchini Syria.
Uvamizi mpya wa Israel dhidi ya Syria unajiri muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa utawala huo batili, Benjamin Netanyahu kufanya safari isiyo ya kawaida katika Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.