Kikao cha UN kuhusu Syria chamalizika bila ya kufikiwa natija
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika jana mjini New York kujadili hali ya kibinadamu nchini Syria kimemalizika bila ya kufikia natija yoyote.
Kikao hicho kilikuwa kimeitishwa na taasisi za misaada ya kibinadamu kutokana na hali mbaya inayoendelea kuwapata watu wa Syria.
Kikao hicho cha Baraza la Usalama kimefanyika baada ya ndege za kivita za kile kinachoitwa muungano wa kimataifa dhidi ya ugaidi unaoongozwa na Marekani kufanya mashambulizi mapema jana Alkhamisi dhidi ya makao ya jeshi la Syria katika mji wa Deir Al Zour mashariki mwa nchi hiyo katika jitihada za Marekani na washirika wake za kuyaunga mkono na kuyasaidia makundi ya kigaidi. Mashambulizi hayo ambayo yametajwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria kuwa ni jinai ya kivita, yameua au kujeruhi zaidi ya askari mia moja wa jeshi la Syria.
Jana usiku Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ilimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la umoja huo ikisisitiza kuwa mashambulizi hayo yamedhihirisha tena utambulisho muovu wa Marekani na malengo yake machafu dhidi ya mamlaka ya kujitawala kwa Syria na watu wake.
Serikali ya Syria imeandika barua kadhaa kwa Katibu Mkuu wa UN na Baraza la Usalama la umoja huo ikitaka kukomeshwa jinai za muungano wa Marekani katika nchi hiyo.