Apr 01, 2018 17:21 UTC
  • Waingereza waandamana kuonyesha mshikamano wao na Wapalestina

Wananchi na makundi ya kiraia katika mji wa London nchini Uingereza wamefanya maandamano wakitangaza uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina na kulaani jinai wanazofanyiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Harakati inayounga mkono Intifadha ya Palestina na baadhi ya makundi mengine ya kiraia yameandamana mjini London na kuyataka mashirika na mabenki ya nchini Uingereza yauwekee vikwazo utawala ghasibu wa Israel. 

Wafanya maandamano hao wamekusanyika mbele ya ubalozi wa Israel mjini London kutangaza uungaji mkono wao kwa haki ya wananchi wa Palestina ya kurejea makwao na kutaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo watoto wa Kipalestina waliotiwa mbaroni na utawala wa Kizayuni. 

Makundi hayo yametangaza pia uungaji mkono wao kwa mapambano ya Intifadha ya Palestina na kuitaka serikali ya Uingereza isitishe uungaji mkono wake kwa utawala huo ghasibu kutokana na tabu na masaibu yanayowapata wananchi wa Palestina na vitendo vya kidhulma wanavyofanyiwa na utawala wa Kizayuni.

Juzi Ijumaa Wapalestina zaidi ya elfu kumi walifanya maandamano makubwa katika mpaka wa Ukanda wa Gaza chini ya anwani "Haki ya Kurejea" .  

Wananchi wa Palestina wakiandamana katika siku ya ardhi na haki ya kurejea huko Ghaza

Siku hiyo jeshi la utawala wa Kizayuni lilituma wanajeshi zaidi ya elfu tatu katika eneo hilo na kuanza kuwafyatulia risasi, kuwanyunyizia gesi ya kutoa machozi na kuwatupia maguruneti waandamanaji. Katika mapigano hayo utawala huo haramu uliwauwa shahidi Wapalestina 17 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 1400.

Maandamano hayo yanatazamiwa kuendelea hadi "Siku ya Nakba" yaani siku ulipoasisiwa utawala bandia na haramu wa Israel.  

Tags