Maafisa wanne wa jeshi la Saudia waangamizwa katika mkoa wa 'Asir
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43362-maafisa_wanne_wa_jeshi_la_saudia_waangamizwa_katika_mkoa_wa_'asir
Maafisa wanne wa jeshi la Saudi Arabia wameangamizwa katika shambulio la ufyatuaji risasi lililotokea kwenye kituo kimoja cha upekuzi mkoani 'Asir kusini magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2018 23:43 UTC
  • Maafisa wanne wa jeshi la Saudia waangamizwa katika mkoa wa 'Asir

Maafisa wanne wa jeshi la Saudi Arabia wameangamizwa katika shambulio la ufyatuaji risasi lililotokea kwenye kituo kimoja cha upekuzi mkoani 'Asir kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imethibitisha habari ya kuuawa maafisa wanne wa jeshi katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika njia inayounganisha miji ya al Mujaradah na Bariq mkoani 'Asir na kutangaza kuwa utambulisho wa baadhi ya washambuliaji hao umeshajulikana.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imedai kuwa: wahusika wawili wa shambulio dhidi ya kituo cha upekuzi wametiwa mbaroni na juhudi zinaendelea kufanywa ili kuweza kumkamata mhusika wa tatu.

Mji wa Bariq uko umbali wa kilomita 930, na ule wa al Mujaradah uko umbali wa kilomita 890 kusini magharibi mwa Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia.

Hadi sasa hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulio hilo.

Kitambo nyuma pia mtu mmoja mwenye silaha asiyejulikana alishambulia kikosi cha doria cha askari usalama wa Saudi Arabia katika mji wa Taif magharibi mwa nchi hiyo. Askari mmoja aliuawa na mwengine alijeruhiwa katika shambulio hilo.../