Utawala wa Aal Saud wawapiga marufuku mahujaji kuzuru "Pango la Hira"
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43494-utawala_wa_aal_saud_wawapiga_marufuku_mahujaji_kuzuru_pango_la_hira
Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imepiga marufuku mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah kuzuru maeneo ya Mlima Nuru na Pango la Hira.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 22, 2018 03:37 UTC
  • Utawala wa Aal Saud wawapiga marufuku mahujaji kuzuru

Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imepiga marufuku mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah kuzuru maeneo ya Mlima Nuru na Pango la Hira.

Wizara ya Hija na Umra ya Saudia imeziamuru taasisi na mashirika yote yanayojishughulisha na masuala ya Hija yasiwaruhusu mahujaji na wafanyaziara kwenda kuzuru Mlima Nuru na kuyataka yafute kwenye ratiba zao safari ya kupeleka mahujaji kwenda kuzuru Pango la Hira.

Naibu Waziri wa Hija na Umra wa Saudi Arabia Abdulaziz al-Wazzan amedai kuwa uamuzi huo umechukuliwa ili kulinda afya na usalama wa mahujaji na kuepusha kufanywa baadhi ya vitendo vinavyopingana na sheria za dini.

Al Azzan amedai kwamba, kutokana na urefu mkubwa wa Mlima Nur kuna hatari ya mahujaji wanaopanda huko kupoteza fahamu au kukumbwa na tatizo la kupumua kutokana na uhaba wa oksijini.

Mlima wa Jabalun-Nur uko umbali wa kilomita nne kaskazini mashariki mwa mji wa Makka na kando ya njia inayotoka Mina kuelekea Arafat. Urefu wa mlima huo kutoka usawa wa bahari ni mita 621 tu na uko katika eneo lenye upana wa mita 281.

Mandhari ya Mlima Nuru

Pango la Hira, mahali alipokuwa akipatumia Bwana Mtume Muhammad SAW kufanyia ibada lipo kwenye kilele cha milima huo wa Jabalun-Nur. Ni ndani ya pango hilo la kihistoria, Bwana Mtume SAW aliteremshiwa Wahyi wa kupewa Utume.

Utawala wa Aal Saud ambao unafuata idiolojia ya Uwahabi umekuwa siku zote ukipinga ada na desturi za Kiislamu na kufanywa ziara ya kuzuru maeneo matukufu ya Makka na Madina.

Tangu mwaka 1924, miji hiyo miwili mitakatifu imekuwa kwenye udhibiti wa utawala huo wa ukoo wa Ibn Saud. Tokea zama hizo hadi sasa miji hiyo ya kihistoria ya Makka na Madina inaandamwa na njama hatari ya kubomolewa na kuharibiwa kupitia mkakati maalumu ulioandaliwa na Mawahabi.

Hadi sasa athari na turathi nyingi za kihistoria za zama za mwanzoni mwa Uislamu zilizokuwepo katika miji hiyo miwili mitakatifu zimebomolewa na utawala wa Aal Saud.../