Kiongozi wa Baraza la Kisiasa Yemen auawa katika hujuma ya Saudia
Kiongozi wa Baraza Kuu la Kisiasa Yemen, Saleh Saleh al-Sammad ameuawa katika hujuma ya ndege za kivita za Saudia Arabia katika mkoa wa al-Hudydah.
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Masirah, al-Sammad, ambaye ni miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Ansarullah, aliuawa katika hujuma ya ndege za kivita za Saudia siku ya Alhamisi.
Harakati ya Ansarullah imesema imemteua Mahdi al Mashat kuchukua nafasi ya Shahidi Al-Sammad.
Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah Sayyid Abdul-Malik Badreddin al-Houthi amehutubia taifa na kulaani vikali jinai hiyo ya Saudia huku akisema Wayemen watalipiza kisasi. Amesema kuuawa Shahidi al-Sammad hakutaathiri hata kidogo harakati ya Wayemen katika mapambano yao dhidi ya uvamizi wa Saudia.
Ikumbukwe kuwa mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ilianzisha vita vikubwa vya kivamizi dhidi ya nchi masikini ya Kiarabu ya Yemen kwa baraka kamili za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu kama vile Imarati na Sudan.
Hadi sasa Wayemen zaidi elfu 14,000 wameuawa huku malaki ya wengine wakijeruhiwa katika hujuma hiyo ya Yemen. Aidha mamilioni ya Wayemen wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na vita hivyo hivyo vya Saudia.
Wakati walipoanzisha uvamizi huo, wavamizi hao wa Yemen walikuwa na ndoto za kuvimaliza muda mfupi sana vita hivyo, hata hivyo uvamizi huo umeingia katika mwaka wake wa nne hivi sasa na bado Saudia imeshindwa kufikia malengo yake ndio maana inamalizia hasira zake kwa kushambulia maeneo ya raia baada ya kuona jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi vimezidi kuwa na nguvu na vinaendelea kuyapiga kwa makombora maeneo ya Saudi Arabia hata mji mkuu wake Riyadh.