Saudia yawashambulia Wayemen wakati maelfu wakimzika kiongozi wao + Video
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43770-saudia_yawashambulia_wayemen_wakati_maelfu_wakimzika_kiongozi_wao_video
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen, leo wamemiminika katika mitaa ya mji mkuu Sana'a kushiriki katika maziko ya kiongozi wa ngazi za juu wa harakati ya wananchi ya Answarullah aliyeuliwa shahidi na ndege za kivita za utawala vamizi wa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 28, 2018 11:48 UTC

Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen, leo wamemiminika katika mitaa ya mji mkuu Sana'a kushiriki katika maziko ya kiongozi wa ngazi za juu wa harakati ya wananchi ya Answarullah aliyeuliwa shahidi na ndege za kivita za utawala vamizi wa Saudi Arabia.

Makumi ya maelfu ya wananchi hao kutoka mikoa mbalimbali ya Yemen wamemiminika katika uwanja wa Sabiini mjini Sana'a licha ya utawala wa Aal Saud kufanya mashambulizi kwenye uwanja huo jana na leo ili kuwatia hofu wananchi hao wasijitokeze kwenye maziko hayo. 

Televisheni ya al Mayadeen ya nchini Lebanon imeripoti kuwa, leo Saudi Arabia imefanya shambulizi la anga karibu na eneo la maziko ya kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Answarullah, Saleh al Sammad, hata hivyo jinai hiyo ya Saudia haikuwatia hofu wananchi wanamuqawama wa Yemen na wamejitokeza kwa wingi mno katika maziko hayo ya leo.

Televisheni hiyo imeongeza kuwa, vikosi vya Yemen vimefanya mashambulizi manane ya makombora ya balestiki katika maeneo ya kiuchumi na nyeti ya Saudi Arabia katika eneo la Jizan, kujibu jinai hizo za ukoo vamizi wa Aal Saud.

Taarifa zinasema kuwa makombora yote manane yamepiga shabaha kwa ustadi mkubwa. Hata hivyo Saudi Arabiya TV imeinukuu wizara ya ulinzi ya Saudi Arabia ikidai kuwa imefanikiwa kutungua makombora manne. 

Sammad aliuliwa shahidi akiwa mstari wa mbele wa mapambano katika mkoa wa al Hudaida. Kiongozi mkuu wa Answarullah, Abdul Malik Badreddin al Houthi amezishutumu Marekani na Saudi Arabia kwa kushirikiana kutenda jinai hiyo na ameahidi kuwa haitapita vivi hivi bila ya kujibiwa.