Saudia: Tunaunga mkono kuwekewa vikwazo zaidi Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43830-saudia_tunaunga_mkono_kuwekewa_vikwazo_zaidi_iran
Adel al Jubeir, waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia amesema kuwa Riyadh inaunga mkono kuwekewa vikwazo zaidi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 29, 2018 22:11 UTC
  • Saudia: Tunaunga mkono kuwekewa vikwazo zaidi Iran

Adel al Jubeir, waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia amesema kuwa Riyadh inaunga mkono kuwekewa vikwazo zaidi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Al Jubeir amesema hayo katika mazungumzo na waandishi wa habari aliyoyafanya akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo, wakati akiwa ziarani nchini Saudi Arabia. Katika mazungumzo hayo, Pompeo amedai kuwa Iran inalipa silaha jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa hiyo na hivyo kuvuruga usalama wa eneo hili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akisalimiana na mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdul Aziz mjini Riyadh

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aidha amedai kuwa nchi yake itaendelea kuzungumza na nchi za Ulaya ili kuhakikisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA yanafanyiwa marekebisho.

Matamshi ya mawaziri hao wawili wa mambo ya nje wa Marekani na Saudi Arabia yametolewa katika hali ambayo katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizo mbili zimekuwa zikiyaunga mkono kikamilifu magenge ya kigaidi kwa kuyapa fedha, silaha na mafunzo ya kijeshi. Genge kama la Daesh lililofanya jinai kubwa katika nchi za Iraq, Syria, Yemen, Libya, Misri na kwengineko ni matunda ya ushirikiano wa Saudi Arabia na Marekani na ni ushahidi tosha wa namna nchi hizo zinavyohatarisha usalama wa eneo hili zima na kumwaga damu za watu wasio na hatia.

Jinai zote zinazofanywa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa nchi maskini ya Kiarabu ya Yemen zinatokana na silaha na zana za kijeshi inazopewa Riyadh na Marekani na madola mengine ya kibeberu, lakini pamoja na hayo yote, madola hayo yanajipa uthubutu wa kuzituhumu nchi nyingine kuwa eti ndizo zinazohatarisha usalama wa eneo hili.