Askari wa Kizayuni wamewatia nguvuni mamia ya watoto wa Kipalestina
Askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewatia nguvuni watoto 1,899 wa Kipalestina tangu ilipoanza Intifadha ya Quds hadi sasa.
Kamati inayoshughulikia masuala ya Wapalestina wanaoshikiliwa na walioachiwa huru kutoka kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni imetoa taarifa maalumu kwa mnasaba wa Siku ya Mtoto wa Palestina na kueleza kuwa tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mnamo mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa, watoto 1,899 wa Kipalestina wametiwa nguvuni na askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni. Taarifa ya kamati hiyo imeongeza kuwa kiwango hicho ambacho hakijawahi kushuhudiwa ni sawa na asilimia 37 ya Wapalestina wote waliotiwa nguvuni na askari wa utawala haramu wa Israel katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo utawala wa Kizayuni umewafunga jela pia watoto 450 wa Kipalestina wenye umri kati ya miaka 12 hadi 18, ambapo mtoto mwenye umri mdogo zaidi miongoni mwa wafungwa hao ni Deyma Al-Wawi, msichana mwenye umri wa miaka 12.
Aidha imeelezwa kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni linatumia mbinu za kinyama za mateso dhidi ya watoto hao na kwamba hatua hizo zisizo za kibinadamu huacha athari mbaya kimwili, kiroho na kiakili kwa watoto hao.
Wakati huohuo Wizara ya Habari ya Palestina imetangaza kuwa kila mwaka utawala wa Kizayuni huwatia mbaroni watoto takribani 700 wa Kipalestina kwa kisingizio cha kuwashambulia kwa mawe askari pamoja na walowezi wa Kizayuni.../