Misri yafungua kivuko cha Rafah kwa ajili ya Ramadhani
Misri imefungua tena kivuko cha Rafah, njia pekee inayotumiwa kufikishia misaada ya dharura kwa Wapalestina karibu milioni mbili walio chini ya mzingiro huko Ukanda Gaza tangu mwaka 2007 na kusema kuwa eneo hilo la mpakani litasalia wazi katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Hayo yamesemwa na Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri katika ujumbe aliotuma jana Alkhamisi katika ukurasa wake wa Facebook na kuongeza kuwa, "Uamuzi huu umefikiwa kwa lengo la kuwapa ahueni wananchi wa Palestina wanaoishi chini ya mzingiro."
Misri imetangaza kukifungua kivuko hicho cha kistratajia siku chache baada ya wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuwaua shahidi Wapalestina 64 na kujeruhi wengine zaidi ya 2,500 waliokuwa wakishiriki maandamano ya amani katika Ukanda wa Gaza, kushinikiza haki ya wao kurejea katika ardhi zao zilizoghusubiwa sanjari na kulaani hatua ya Marekani ya kuhamishia ubalozi wake katika mji wa Quds Tukufu, kutoka Tel Aviv.
Hatua ya serikali ya Misri ya kukifunga kivuko cha Rafah ambayo ndiyo njia pekee ya kuingilia na kutokea wakaazi wa Gaza imesababisha masaibu na matatizo makubwa ya kibinadamu na kiuchumi kwa Wapalestina wapatao milioni moja na laki tisa wanaoishi katika eneo hilo.
Ukanda wa Gaza uko chini ya mzingiro wa nchi kavu, anga na baharini wa utawala haramu wa Kizayuni tangu mwaka 2006 na hivyo kusababisha matatizo chungu nzima kwa wakazi wa eneo hilo.