Saudia yashadidisha vita dhidi ya Yemen katika Mwezi wa Ramadhani
Saudi Arabia imeshadidisha mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya raia nchini Yemen katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Masirah, ndege za kivita za muungano wa Saudia, zimeshadidisha mashambulizi dhidi ya shule, nyumba za makazi, misikiti na maeneo mengine ya umma nchini Yemen katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Ripoti hiyo imesema ndege za kivita za Saudia hivi karibuni zilivurumisha mabomu katika mji wa Baqim katika mkoa wa Saada kaskazini mwa Yemen. Katika hujuma hiyo, raia kadhaa wa Yemen wameuawa na kujeruhiwa.
Taswira za vidoe kutoka Saada zinaonyesha ndege za Saudia zikilenga mashamba na kusababisha hasara kubwa.
Televisheni ya Al Masirah pia imeripoti kuwa, katika mwezi uliopita wa Mei, wanajeshi 55 wa Saudi Arabia waliuawa kufuatia mashambulizi ya wapiganaji wa Yemen katika maeneo ya Najran, Jeizan na Asir kusini mwa Saudi Arabia. Aidha wanajeshi wengine 50 wa ufalme huo walijeruhiwa katika mapigano hayo. Vyombo vya habari vya Saudi vimekiri kuwa katika mapigano hayo askari 75 Wasaudi waliuawa au kujeruhiwa.
Ikumbukwe kuwa Saudia ilianzisha hujuma yake dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu urais na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh, ambapo watu zaidi ya 14,000 wameuawa na mamilioni ya wengine kujeruhiwa.
Katika kukabiliana na jinai hizo, wanajeshi wa Yemen wamekuwa wakitumia makombora yaliyoundwa nchini humo kushambulia maeneo kadhaa ya kijeshi na kiuchumi ya Saudi Arabia ukiwemo mji mkuu wa nchi hiyo, Riyadh.