Saudia yadondosha mabomu katika kituo cha tiba nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i45756-saudia_yadondosha_mabomu_katika_kituo_cha_tiba_nchini_yemen
Ndege za kivita za Saudi Arabia zimedondosha mabomu katika kituo kimoja cha afya cha kuwatibu watu wenye kipindupindu nchini Yemen ambacho kinasimamiwa na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2018 09:14 UTC
  • Saudia yadondosha mabomu katika kituo cha tiba nchini Yemen

Ndege za kivita za Saudi Arabia zimedondosha mabomu katika kituo kimoja cha afya cha kuwatibu watu wenye kipindupindu nchini Yemen ambacho kinasimamiwa na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).

Kufuatia hujuma hiyo ya Jumatatu iliyopelekea watu wasiopungua saba kuuawa katika mji wa Abs kaskazini magharibi mwa Yemen katika mkoa wa Hajjah, MSF imesema imesitisha kwa muda huduma zake katika eneo hilo.

Katika taarifa, mkuu wa MSF nchini Yemen amesema hujuma hiyo ya Jumatatu asubuhi dhidi ya kituo cha MSF cha kutibu kipindupindu, ilitekelezwa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia pamoja na Imarati na ni ishara ya kutoheshimu vituo vya tiba na wagonjwa. 

MSF imesema inasitisha huduma zake huko Abs hadi pale itakapopata dhamana ya usalama wa wafanyakazi wake na wagonjwa. Wakuu wa MSF wanasema Saudia ilikuwa imefahamishwa eneo hilo ni la kutoa matibabu lakini imeamua kudondosha mabomu katika kituo hicho cha matibabu, jambo ambalo linahesabiwa kuwa jinai ya kivita.

Ndege ya kivita ya Saudia ikielekea katika oparesheni

Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi makali ya kikatili dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen mwezi Machi 2015 kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Imarati na kwa kutumia silaha zinazopewa na nchi za Magharibi.

Hadi hivi watu karibu 15,000, wengi wakiwa ni watoto na wanawake wameshauawa na makumi ya maelefu ya wengine kujeruhiwa huko Yemen na mamilioni wakiachwa bila makao. Aidha hujuma hiyo ya Saudia, ambayo inapata himaya ya utawala haramu wa Israel, Uingereza na Marekani, imepelekea Yemen kukumbwa pia na janga la umaskini, ukame na miripuko ya magonjwa mbalimbali hatari ya kuambukiza kama vile kipindupindu.