Utawala wa Bahrain wawahukumu kifo wanazuoni watatu wa Kiislamu
Mahakama ya utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain imetoa hukumu ya adhabu ya kifo dhidi ya wanazuoni watatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo kwa tuhuma bandia dhidi yao, ikiwa ni muendelezo wa hukumu zisizo za kiuadilifu zinazotolewa na watawala madikteta wa nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
Harakati ya Kitaifa ya Kiislamu ya al-Wefaq ambalo ndilo kundi kubwa zaidi la upinzani nchini Bahrain imetoa taarifa inayosema kuwa, wanazuoni hao watatu wamehukumiwa adhabu ya kifo, huku wengine wanane wakihukumiwa kifungo cha maisha jela.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, harakati hiyo kufikia sasa imerekodi kesi 347 za kukamatwa wanaharakati wa upinzani nchini humo wakiwemo wanazuoni 99 wa Kishia, mbali na kuwaita wengine 156 kuwasaili kutokana na hotuba zao au misimamo yao ya kisiasa.
Aidha wanazuoni wengine wengi wa Kiislamu nchini Bahrain wamepokonywa uraia na watawala wa Manama kutokana na harakati zao za kisiasa.
Tangu Februari 14 mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kiukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.
Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.