Msafara wa vifaru vya Saudia waangamizwa na Wayemen
Kikosi cha mizinga na makombora cha jeshi pamoja na Harakati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen, kimefanikiwa kuangamiza msafara wa vifaru vya Saudi Arabia vilivyokuwa ndani ya ardhi ya nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Yemen pamoja na harakati hiyo ya wananchi imesema kuwa, vifaru hivyo vya adui vimeangamizwa katika mji wa Najran, kusini mwa Saudia na upande wa magharibi wa kambi ya kijeshi ya al-Sadis. Imesema kuwa, baada ya kufuatilia na kubaini msafara huo wa vifaru na magari ya deraya, jeshi la Yemen na harakati ya Answarullah liliushambulia msafara huo na kuusambaratisha. Duru za kijeshi zimefichua kuwa, katika shambulizi hilo, askari wengi wa Saudia na vibaraka wake wameangamizwa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Wakati huo huo, jeshi la Yemen limefanikiwa kuangamiza pia idadi kadhaa ya askari wa Saudia na vibaraka wake katika mkoa wa Al Bayda eneo la Qania.
Mbali na hayo jeshi la Yemen na harakati hiyo ya wananchi limefanya operesheni katika eneo la Naham la mkoa wa Sana'a, mji mkuu wa nchi hiyo na kufanikiwa kuangamiza wanamgambo wenye mfungamano na Abdrabbuh Mansur Hadi, rais kibaraka wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu nafasi hiyo na kisha kutoroka nchi. Kwa mujibu wa habari hiyo, operesheni hizo zimefanyika katika miinuko ya al-Riyah na al-Iyashat ambapo wanamgambo kadhaa vibaraka wameangamizwa na kujeruhiwa. Hayo yanajiri katika hali ambayo Alkhamisi iliyopita kikosi cha Anga cha Jeshi la Yemen kilifanikiwa kudungua ndege ya kivita ya Saudi Arabia, kusini mashariki mwa ardhi ya Saudia. Wizara ya Ulinzi ya Yemen imesema vikosi vya Yemen vilitungua ndege hiyo ya Saudia katika eneo la Asir, kusini mashariki mwa Saudi Arabia, ikitokea mkoa wa Sa'ada, kaskazini mwa Yemen.