Umoja wa Mataifa wataka kuhitimishwa mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza
Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Mashariki ya Kati ametoa wito wa kuhitimishwa mzingiro wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Nickolay Mladenov amesema kuwa, hali ya mambo katika Ukanda wa Gaza ni ya "maafa" na kuongeza kuwa, wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo ya uhaba wa umeme na maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Mashariki ya Kati ameunga mkono pia maandamano ya amani ya wananchi wa Ukanda wa Gaza ya "Haki ya Kurejea" na kuutaka utawala ghasibu wa Israel kuuacha kuwafyatulia risasi watoto.
Tangu Januari mwaka 2006 na kufuatia ushindi wa harakati ya Hamas katika uchaguzi wa Bunge la Palestina, utawala wa Kizayuni wa Israel uliliwekea eneo la Ukanda wa Gaza mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu kwa lengo la kuisambaratisha harakati hiyo ya muqawama.
Mzingiro huo unazuia kuingizwa katika eneo la Gaza bidhaa za mahitaji ya msingi zikiwemo za fueli, dawa na vifaa vya ujenzi.
Nchi nyingi duniani ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na asasi za kimataifa zimeendelea kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel ikiwemo hatua yake ya kulizingira eneo la Ukanda wa Gaza na kuzuia kufikishiwa wananchi wa eneo hilo bidhaa muhimu kama chakula na dawa. Kwa sasa eneo hilo limo hatarini kukabiliwa na maafa ya kibinadamu kutokkana na kukosekana huduma muhimu.