Saudi Arabia yasimamisha kupitishia mafuta na meli zake Babul Mandab
Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia Khalid al Falih ametangaza kuwa usafirishaji mafuta wa nchi hiyo kupitia Lango Bahari la Babul Mandab unasimamishwa hadi hapo kutakapokuwa na hakikisho la usalama wa majini.
Uamuzi huo umechukulwia baada ya kikosi cha majini cha Jeshi la Yemen kuzishambulia manowari mbili za muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika pwani ya magharibi mwa nchi hiyo katika muda wa chini ya masaa 24.
Matukio ya Yemen yanaonyesha kuwa wanamapambano wa harakati ya Ansarullah wanafanya jitihada kubwa za kulinda usalama na nchi yao na askari vamizi hawana njia nyingine ya kujinusuru mbele ya wanamuqawama hao wa Yemen ghairi ya kusimamisha mashambulizi yao, kuacha kuizingira Yemen na kuziondoa meli zao za kivita katika bandari za nchi hiyo. Kamanda wa Jeshi la Majini la Yemen ameeleza kuwa wanajeshi vamizi wa Saudi Arabia na Marekani ndio wanaotishia amani na usalama wa kimataifa na kuhatarisha usalama wa Bahari Nyekundu.
Oparesheni za aina yake za jeshi la majini la Yemen dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na vikosi vamizi zimeleta mabadiliko makubwa katika mapambano ya Wayemeni dhidi ya askari vamizi. Uwezo na nguvu kubwa ya wanamapambano wa Yemen katika nyuga mbalimbali ikiwemo katika kutekeleza mashambulizi ya baharini yamevuruga kikamilifu mlingano wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia huko Yemen.
Lango la Babul Mandab ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za baharini duniani katika Ghuba ya Aden, na hapana shaka kwamba miongoni mwa malengo ya Saudi Arabia kuishambulia Yemen ni kutaka kujitanua na kuidhibiti njia hiyo muhimu ya baharini. Lango Bahari la Babul Mandab lina mchango mkubwa pia katika kusafirisha nishati duniani. Lango bahari la kistratejia la Babul Mandab linapatikana kati ya nchi za Yemen. Djibouti na Eritrea.
Kuwepo Yemen katika Lango Bahari la Babul Mandab ambalo ni makutano ya Bahari Nyekundu na ile ya Hindi kumeipa nchi hiyo nafasi maalumu ya kistratejia. Kwa upande wa usalama, eneo hilo pia lina umuhimu kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na vilevile lina umuhimu katika kulinda usalama wa vituo vya Marekani huko katika Pembe ya Afrika na katika kupitishia meli zilizobeba mafuta ya Saudia yanayosafirishwa katika maeneo mbalimbali duniani; kwa msingi huo kuizingirwa eneo hilo na Saudia kunaweza kuwa na nafasi muhimu katika kulinda maslahi hayo ya pamoja. Katika uga huo tunaweza kusema kuwa, utawala wa Aal Saud umeshindwa pia kutimiza malengo yake ya kistratejia yaani kulidhibiti Lango Bahari la Babul Mandab baada ya kushindwa kufikia malengo yake ya kisiasa iliyoyakusudia ikiwemo kumrejesha madarakani kibaraka wake, rais mstaafu wa Yemen Abdu Rabbu Mansour Hadi.
Gazeti la al Akhbar linalochapishwa Lebanon limeandika kuwa: Kuendelea mapambano ya Wayemeni na kupanuka zaidi hadi kujiri mashambulizi ya baharini kati ya wanamapambano wa Yemen na vikosi vamizi kumesambaratisha njama zilizokuwa zimeratibiwa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudia tangu miezi kadhaa iliyopita ambapo lengo la mpango huo lilikuwa kuidhibiti eneo la Babul Mandab.
Kushindwa huko kumetokea huku Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vyake dhidi ya Yemen hususan katika jitihada zake za kutaka kulidhibiti Lango Bahari la Babul Mandab.