Indhari za kimataifa; Yemen katika maafa ya kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47233
Kufuatia kushtadi mashambulizi ya vikosi vamizi vya Saudi Arabia na waitifaki wake huko Yemen, taasisi za misaada ya kibinadamu za kimataifa zimetahadharisha kuhusu kutokea maafa ya kibinadamu nchini humo khususan katika bandari iliyokumbwa na mgogoro ya al Hudaydah.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 05, 2018 02:30 UTC
  • Indhari za kimataifa; Yemen katika maafa ya kibinadamu

Kufuatia kushtadi mashambulizi ya vikosi vamizi vya Saudi Arabia na waitifaki wake huko Yemen, taasisi za misaada ya kibinadamu za kimataifa zimetahadharisha kuhusu kutokea maafa ya kibinadamu nchini humo khususan katika bandari iliyokumbwa na mgogoro ya al Hudaydah.

Indhari ya karibuni kabisa imetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la  Idadi ya Watu (UNFPA) ambalo limeeleza wasiwasi wake kuwa mamia ya akinamama wajawazito wanakabiliwa na ukosefu wa huduma za tiba na wako katika hatari ya kuaga dunia. Shirika hilo limeripoti kuwa kiwango cha vifo vya akinamama wa Kiyamani kimeongezeka mara mbili sasa ikilinganishwa na mwaka 2015.  

Aidha Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umetahadharisha kuhusu kukosekana usalama wa chakula kwa raia wa Yemen milioni 18 walioathiriwa na vita.  Kama alivyosema Lise Grande Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa; Wayamani milioni nane na nusu wanatabika na njaa kali; hiyo ikiwa na maana kuwa raia hao hupata mlo mmoja tu wa chakula kwa siku au kila baada ya siku mbili.  

Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuhusu kushuhudiwa wimbi jipya la utapiamlo na mlipuko wa maradhi ya kipindupindu huko Yemen na kueleza kuwa Yemen inakabiliwa na wimbi la kuenea kwa kasi na kwa hatari maambukizo ya kipindupindu mbali na kuongezeka idadi ya vifo vya watu kutokana na njaa. Hayo yote yanasababishwa na kuharibiwa mifumo ya usambazaji maji na hospitali katika mashambulizi yanayotekelezwa na Saudi Arabia nchini humo. Aidha hali ya watoto huko Yemen ni mbaya sana.

Watoto wa Kiyamani wakisubiri mgao wa chakula