Umoja wa Mataifa wakaribisha taarifa ya Hamas kuhusu usitishaji vita Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i131574-umoja_wa_mataifa_wakaribisha_taarifa_ya_hamas_kuhusu_usitishaji_vita_gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kwa mikono miwili taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas inayoonyesha utayarifu wake wa kuwaachilia mateka na kukubali kwa masharti mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-10-17T02:15:18+00:00 )
Oct 04, 2025 07:31 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakaribisha taarifa ya Hamas kuhusu usitishaji vita Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kwa mikono miwili taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas inayoonyesha utayarifu wake wa kuwaachilia mateka na kukubali kwa masharti mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres "anatoa wito kwa pande zote kuchukua fursa hiyo ili kumaliza mzozo wa Gaza," Stephane Dujarric, Msemaji wa Guterres amesema katika taarifa.

Kauli yake imekuja baada ya afisa mwandamizi wa Hamas, Mousa Abu Marzouk kusema Ijumaa kwamba, kundi la Muqawama la Palestina limekubali mpango wa Trump wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa, huku akisisitiza kwamba utekelezaji wake utahitaji mazungumzo.

"Guterres anazishukuru Qatar na Misri kwa kazi yao "ya thamani" ya upatanishi kwenye mgogoro wa Gaza," Dujarric amesema.

"Katibu Mkuu anasisitiza wito wake thabiti wa kusitisha mapigano mara moja na ya kudumu, kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote, na ufikishaji usio na vikwazo wa misaada ya kibinadamu," ameongeza. Umoja wa Mataifa utaunga mkono juhudi zote kuelekea malengo haya ili kuzuia mateso zaidi, alisisitiza.

Hamas imetangaza kukubali kukomesha kabisa vita, mabadilishano ya mateka na kutaka kuangaliwa upya mustakabali wa Gaza kwa kuzingatia maslahi mapana ya kitaifa ya Palestina.

Kwa mujibu wa Al-Alam, harakati hiyo imetoa taarifa na kutangaza kwamba jibu hilo la masharti limetolewa baada ya mashauriano ya kina ya ndani ya HAMAS na baina ya makundi ya Wapalestina na wapatanishi wa kieneo.

Katika taarifa hiyo, Hamas, imetilia mkazo wajibu wake wa kitaifa na haja ya kusimamishwa mara moja jinai na mauaji ya umati yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.