Aug 07, 2018 14:33 UTC
  • Utawala wa Aal Khalifa waendelea kubomoa misikiti ya Waislamu wa Bahrain

Utawala wa Aal Khalifa umeendeleza hatua kandamizi dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Bahrain kwa kuubomoa tena msikiti mwengine wa Waislamu hao.

Mabuldoza ya utawala wa Aal Khalifa yamevamia kitongoji cha Az-Zanaj kilichoko kwenye mji mkuu wa Bahrain, Manama na kuubomoa kwa mara nyingine msikiti wa Al-'Alawiyyat.

Hata hivyo baada ya hatua hiyo ya askari wa utawala wa Aal Khalifa, wakazi wa eneo hilo walianza kazi ya kuujenga tena msikiti huo uliobomolewa.

Hapo kabla pia Sheikh Ahmad Amrullah, mjumbe wa kamati kuu ya baraza la maulamaa wa Kiislamu Bahrain alisisitizia kuyahami matukufu ya Kiislamu na kueleza kwamba misikiti inayobomolewa inapasa ijengwe tena.

Waislamu wakisali kwenye eneo ulipobomolewa msikiti wa Al-Alawiyyat

Sheikh Ahmad Amrullah aidha amelaani hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kuendelea kubomoa misikiti na kutoijenga tena; na kutaka waziri wa sheria na askari wa utawala huo wa kiimla wafunguliwe mashtaka kwa kuhujumu matukufu ya kidini ikiwemo kubomoa misikiti na husainiyyah.

Licha ya hatua kali na kandamizi zinazochukuliwa na utawala wa Aal Khalifa, wananchi Waislamu wa Bahrain wanaendelea kutetea haki zao kwa kulaani hatua za utawala huo za kubomoa misikiti, hatua ambazo zinakinzana na sheria za kimataifa. Lakini sambamba na hayo Waislamu hao wanaendelea kusali Sala za jamaa kwenye sehemu za misikiti iliyobomolewa hatua ambayo imesababisha waumini na maimamu wa Sala hizo kutiwa nguvuni au kusailiwa na vyombo vya usalama.../

Tags