Aug 20, 2018 03:55 UTC
  • Kamata kamata yaendelea nchini Saudi Arabia

Birjas Hamoud al Birjas, Mshauri wa zamani wa Kampuni ya Mafuta na Gesi Asilia ya Saudi Arabia (ARAMCO) ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya mafuta nchini humo pia ametiwa mbaroni katika kamatakamata inayoendelea nchini Saudia.

Birjas Hamoud al Birjas ametiwa mbaroni baada ya kukosoa kupanda kwa bei ya nishati na umeme nchini Saudia.

Mshauri huyo wa zamani wa masuala ya uchumi katika kampuni ya Aramco aliwahi pia kuikosoa serikali kuhusu ukosefu wa ajira na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini humo.

Ripoti zinasema kuwa askari usalama wa Saudi Arabia wanajiandaa kwa ajili ya kusikilizwa kesi ya vigogo wanane wa nchi hiyo waliotiwa mbaroni wakiwemo maulamaa wa kidini. 

Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia

Wakati huo huo taasisi za kisheria za kimataifa zimetaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo wale wote waliotiwa mbaroni huko Saudi Arabia na zimetaka kutangazwa mahali watu hao wanaposhikiliwa.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita khususan baada ya kuteuliwa Muhammad bin Salman kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ambaye anafuata siasa za Marekani na Israel, makumi ya wafanyabiashara, wanazuoni, wanawafalme na maulamaa wa nchi hiyo wametiwa mbaroni na kufungwa jela.

Tags