Syria yaitaka Hizbullah iendelee kubakia nchini humo
Serikali ya Syria imeitaka Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanona iendelee kubakisha wapiganaji wake nchini humo, baada ya kumalizika mapigano ya kijeshi kaskazini mwa nchi.
Habari zinasema kuwa, tayari harakati hiyo imepokea rasmi ombi la viongozi wa serikali ya Syria juu ya udharura wa kusalia wapiganaji wake nchini humo hata baada ya kumalizika operesheni katika maeneo ya kaskazini magharibi na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Gazeti la al-Akhbar la nchini Lebanon sambamba na kuashiria kuwa, harakati hiyo tayari ilikuwa imechukua hatua za ndani kwa ajili ya kubakisha wapiganaji wake kwa muda mfupi nchini Syria, limeandika kuwa, wapiganaji wa muqawama watakuwa na nafasi chanya katika kuwasaidia viongozi wa Syria sambamba na kurejea nyumbani wakimbizi wa nchi hiyo kutoka Lebanon na kadhalika kuratibu hali ya mambo katika mipaka ya pamoja kati ya nchi mbili.
Kabla ya hapo pia Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon alikosoa baadhi ya mapendekezo ya pande fulani ya kutaka kuondoka harakati hiyo Syria na kusisitiza kuwa, kwa kuzingatia hali ya sasa ya Syria, kuondolewa wapiganaji wa muqawama wa Hizbullah ambao wapo Syria kwa ombi rasmi la serikali ya Damascus, sio jambo la busara.