Saudi Arabia yaizuia meli iliyobeba mafuta iliyokuwa ikielekea Yemen
Muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia umeizuia meli moja iliyokuwa imepakia bidhaa za mafuta iliyokuwa ikielekea katika bandari ya al Hudaydah magharibi mwa Yemen.
Duru ya kuaminika katika bandari hiyo imeripoti leo kuwa meli hiyo iliyobeba bidhaa za mafuta kwa ajili ya wananchi wa Yemen ilikuwa na kibali cha Umoja wa Mataifa. Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Marekani na nchi nyingine kadhaa mwezi Machi mwaka 2015 ziliivamia Yemen na kisha kuizingira nchi hiyo baharini, nchi kavu na angani.
Wayemeni zaidi ya elfu 14 wameuawa, makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi hadi sasa tangu Saudia na waitifaki wake waanzishe vita katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Muungano huo vamizi unaoongozwa na Saudia sambamba na kuendelea kuzingira Yemen unazizuia meli za bidhaa za mafuta na ndege zenye misaada ya kibinadamu na madawa kuwasili katika bandari na kutua kwenye viwanja vya ndege vya nchi hiyo na hivyo kuifanya nchi hiyo ikabiliwe na uhaba mkubwa wa chakula na dawa.