Makumi ya walowezi wa Kizayuni wavamia Msikiti wa al-Aqswa
Makumi ya walowezi wa Kizayuni leo wamevamia Msikiti wa al-Aqswa wakiwa wanasaidiwa na askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel na kufanya vitendo vya kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu.
Ripoti zinasema kuwa, polisi ya utawala wa Kizayuni wa Israel iliandaa mazingira ya kiusalama kwa ajili ya kuingia katika eneo hilo walowezi hao wa Kizayuni.
Walowezi hao wa Kizayuni baada ya kuingia katika eneo la Msikiti wa al-Aqswa walisikika wakipiga nara zilizo dhidi ya Uislamu.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa al-Aqswa umeongezeka mno katika siku za hivi karibuni.

Inaelezwa kuwa, karibu kila siku walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakifanya uvamizi katika msikiti huo lengo likiwa ni kutekeleza njama za kutokomeza utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa Msikiti wa al-Aqswa na badala yake kuweka nembo za Kizayuni.
Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya juhudi za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.
Hata hivyo kusimama kidete wananchi wa Palestina hadi sasa kumekwamisha njama na mipango yote ya Wazayuni, zikiwemo njama za kutaka kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa Baytul Muqaddas.