Uhispania yafuta mkataba wa kuiuzia Saudia mabomu 400
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47898-uhispania_yafuta_mkataba_wa_kuiuzia_saudia_mabomu_400
Uhispania imetangaza kubatilisha mkataba wa kuiuzia Saudi Arabia mabomu 400 yenye thamani ya Euro milioni 9.2 kufuatia jinai za hivi karibuni za muungano unaoongozwa na Saudia ambao umeua idadi kubwa ya watoto Wayemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2018 09:06 UTC
  • Uhispania yafuta mkataba wa kuiuzia Saudia mabomu 400

Uhispania imetangaza kubatilisha mkataba wa kuiuzia Saudi Arabia mabomu 400 yenye thamani ya Euro milioni 9.2 kufuatia jinai za hivi karibuni za muungano unaoongozwa na Saudia ambao umeua idadi kubwa ya watoto Wayemen.

Katika taarifa, Wizara ya Ulinzi ya Uhispania imesema itarejesha Euro milioni 9.2 ambazo zilikuwa zimelipwa na Saudia kununua mabomu 400 ya yenye ustadi mkubwa kutokana na hofu kuwa yanaweza kutumiwa kuwaua raia wasio na hatia Yemen.

Uhispania imebadilisha msimamo wake baada ya ndege za kivita za Saudia kushambulia basi la shule ya Qur'ani na kuwaua watu 51 wakiwemo watoto 40. Uhispania imesema pia iko mbioni kutathmini mikataba yake yote ya kuizuia Saudi Arabia silaha.

Kwa mujibu wa Amnesty International, Uhispani ni nchi ya nne katika orodha ya nchi zinazoiuzia Saudi Arabia silaha zingine zikiwa ni Marekani, Uingereza na Ufaransa. Tayari Sweden, Canada, Finland, Norway, Belgium na Ujerumani zimesitisha kwa muda uuzaji silaha kwa Saudia.

Watoto wa Yemen ni waathirika wakuu wa jinai za Saudia dhidi ya Yemen

Muugano wa kivita wa Saudia uliivamia Yemen mwezi Machi mwaka 2015 na hadi sasa watu karibu 15,000 wamepoteza maisha na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi kutokana na uvamizi huo unaopata himaya ya Marekani na utawala haramu wa Israel.