Sep 29, 2018 08:13 UTC
  • Jeshi la Israel laendeleza ukatili wake, laua Wapalestina 7 Gaza

Kwa akali Wapalestina saba wameuawa shahidi huku wengine zaidi ya 500 wakijeruhiwa baada ya jeshi la Israel kuwamiminia risasi na kuvurumishia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza.

Wizara ya Afya ya Gaza imesema Nasser Azmi Musbah, kijana wa miaka 12 na mwenzake wa miaka 14 kwa jina Mohammed Nayef al-Houm ni miongoni mwa Wapalestina waliouawa shahidi baada ya wanajeshi katili wa Israel kushambulia maandamano ya Haki ya Kurejea katika Ukanda wa Gaza jana Ijumaa.

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, watoto 35, wanawake wanne, madaktari wanne na waandishi wa habari kadhaa ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika maandamano hayo.

Maandamano ya amani yaliyopewa jina la "Haki ya Kurejea" yalianza tarehe 30 Machi mwaka huu kwa mnasaba wa Siku ya Ardhi huko Ukanda wa Gaza na yangali yanaendelea.

Wapalestina wakiandamana katika Ukanda wa Gaza

 

Tangu wakati huo hadi sasa zaidi ya Wapalestina 190 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel na wengine 17,500 wamejeruhiwa.

Maandamano hayo yamewatia kiwewe viongozi wa utawala dhalimu wa Israel na ndio maana wamekuwa wakiwafyatulia risasi na mambomu ya kutoa machozi waandamanaji na kuwaua ovyo.

Tags