Oct 12, 2018 16:51 UTC
  • Wabahrain waandamana wakitaka kususiwa uchaguzi

Idadi kubwa ya wananchi wa Bahrain leo wamefanya maandamano kuunga mkono uamuzi wa maulamaa wa nchi hiyo waliotaka kususiwa uchaguzi wa kimaonyesho wa utawala wa Aal Khalifa.

Duru za habari za Bahrain zimeripoti kuwa katika maandamano hayo ambayo yalifanyika eneo la al Deraz wafanya maandamano walikuwa wamebeba picha za Sheikh Issa Qassim mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu na vilevile za mashahidi waliouawa na askari usalama wa nchi hiyo nchi hiyo. Waandamaji ambao wametoa wito wa kususiwa uchaguzi wa bunge wa kimaonyesho ulioandaliwa na utawala wa Aal Khalifa,  walipiga nara dhidi ya hatua ya utawala huo ya kuwazuia wananchi kuswali Sala ya Ijumaa. 

Maandamano hayo yamefanyika leo mjini Manama huku askari usalama wa serikali ya Bahrain wakiendelea kulizingira eneo hilo na nyumba ya Ayatullah Sheikh Issa Qassim kwa wiki ya 118 mtawalia. 

Hussein al Daihi Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al Wifaq ya nchi hiyo Jumanne iliyopita alitangaza habari ya kususia uchaguzi wa bunge na mabaraza ya miji na kuwatolea wito wananchi kususia uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 24 Novemba mwaka huu licha ya utawala wa al Khalifa kutishia kuwa utawaadhibu wale wote watakaosusia uchaguzi huo. 

Hussein al Daihi, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al Wifaq ya Bahrain

 

Tags