Nov 06, 2018 15:07 UTC
  • Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel ameunga mkono muswada unaopendekeza kunyongwa mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za kutisha za utawala huo.

Shirika la habari la Qudsuna limeripoti kuwa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameafiki suala hilo baada ya wakuu wa vyama vinavyounda muungano unatawala Israel kupasisha suala la kunyongwa mateka wa Kipalestina katika kikao kilichoongozwa na Waziri wa Elimu wa utawala huo haramu, Naftali Bennett.

Baada ya Netanyahu na wakuu wa vyama vya muungano tawala kuafiki suala hilo sasa Bunge la Israel, (Knesset) linatazamiwa kuanza kuchunguza muswada wa sheria inayuruhusu kunyongwa mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel. 

Maelfu ya Wapalestina wanashikiliwa kama mateka katika jela za Israel.

Kwa mujibu wa muswada huo uliotayarishwa mwezi Januari mwaka huu, idhini ya kunyongwa mateka wa Kipalestina sasa haitahitaji mwafaka wa majaji watu wa mahakama ya kijeshi na hakuna kiongozi yeyote mwenye haki ya kuzuia utekelezaji wa sheria hiyo. 

Muswada wa kunyongwa mateka wa Kipalestina ulipendekezwa na chama cha Yisrael Beiteinu kinachoongozwa na Waziri wa Vita wa Israel, Avigdor Lieberman. Muswada huo ulipendekezwa kutokana na woga wa kupanuka zaidi upinzani na mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala huo ghasibu. 

Tags