Zaidi ya magaidi 24 wa ISIS wauawa nchini Iraq
Zaidi ya magaidi 24 wa genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) wameuawa katika mashambulizi ya anga na nchi kavu yaliyofanywa kwenye maeneo tofauti na wanajeshi wa Iraq katika opereseheni ya kuyasafisha mabaki ya magaidi hao katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Meja Alaa al Saadi wa Komandi ya Operesheni ya Diyala amesema kuwa, magaidi wanne wa Daesh wameuawa wakati ndege ya kivita ya Iraq iliposhambulia maficho yao katika eneo la Hamrin lililoko umbali wa kilomita 90 kaskazini mwa Baqubah.
Amesema, wanajeshi wa Iraq wanaendelea na operesheni zao za kuwasaka magaidi wa Daesh na kuvunja maficho yao katika eneo hilo.
Wakati huo huo, afisa mmoja wa usalama ambaye hakutaka kutajwa jina lake ameliambia shirika la habari la Iraq kwamba askari wa serikali ya shirikisho ya nchi hiyo wakisaidiwa na ndege za kivita wamefanya operesheni kadhaa katika wilaya za Badush na Hatra katika mkoa wa Nainawa (Nineveh) na kuua zaidi ya magaidi 20 wa Daesh.
Katika upande mwingine, kamanda wa vikosi vya kujitolea vya wananchi, maarufu kwa jina al Hashd al Shaabi huko magharibi mwa mkoa wa al Anbar wa magharibi mwa Iraq amesema kuwa, vikosi hivyo vimeshambulia kwa makombora maeneo ya magaidi wa Daesh ndani ya ardhi ya Syria.
Qassim Muslih amesema, wanamapambano wa al Hashd al Shaabi wameshambulia kwa makombora maeneo ya magaidi wa ISIS katika maeneo ya al Baghur na al Bukamal nchini Syria.
Magaidi wa Daesh wanatumia ardhi ya Syria kupanga mashambulizi dhidi ya maeneo ya Iraq na mara kwa mara wamekuwa wakivuka mpaka wa nchi hizo mbili na kuingia Iraq kufanya vitendo vya kigaidi.